SUMBAWANGA: MCHUNGAJI,WAUMINI WAKESHA WAKIMUOMBEA MAREHEMU AFUFUKE
Picha kwa hisani ya mtandao
MCHUNGAJI na waumini wa Kanisa la The
Evangelistic Assemblies of God (EAGT) mtaa wa Eden 'A' Manispaa ya Sumbawanga,
Rukwa, wamekesha wakimuombea marehemu wao afufuke, wakidai alikufa kwa nguvu ya
giza.
Elizabeth Lwitiko (30) alifariki
dunia juzi saa tatu asubuhi kutokana na matatizo ya uzazi, wakati akijifungua
pacha, aliowaacha hai na wametafutiwa mlezi.
Mchungaji Jacob Lwitiko
aliongoza waumini wake, kuchukua mwili wa marehemu chumba cha kuhifadhi maiti
cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, Sumbawanga na kuiweka kwenye madhabahu
ya kanisa hilo na kufanya maombezi, wakiamini kuwa huenda atafufuka.
Mchungaji Lwitiko ni kaka wa
Elizabeth na aliachiwa uongozi wa kanisa hilo na kaka yake, Amos Lwitiko,
mwanzilishi na kwa sasa yuko Makambako mkoani Njombe. Mwenyekiti wa Mtaa wa
Edeni “A” lililopo kanisa hilo, Gerald Mwazembe alikiri kuwepo kwa mkasa huo,
uliowashitua wakazi wa jirani kwani ni mara ya kwanza kutokea.
Akisimulia, alisema kuwa Elizabeth
alifariki dunia saa tatu asubuhi katika Kituo cha Afya cha Mazwi mjini hapa
kutokana na matatizo ya uzazi, ambapo alipungukiwa damu mwilini baada ya
kujifungua salama kwa njia ya kawaida watoto pacha ambao wako hai.
“Mwili wa marehemu ulihifadhiwa chumba
cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, lakini waombolezaji
na mchungaji wa kanisa hilo waliuchukua mwili huo wakiamini alikufa kishirikina
na kwamba wakimwombea angeweza kufufuka,” alieleza.
Alisema mwili ulipofikishwa kanisani
hapo, uliwekwa madhabahuni na ibada ya maombezi iliyoambatana na nyimbo na
midundo ya ngoma, ilifanyika kuanzia saa sita mchana hadi usiku wa manane huku
milango ikiwa imefungwa, wakiamini kuwa atafufuka.
“Ilipofika usiku wa manane
niliwapigia simu Polisi ambapo askari wa kikosi cha doria walifika kanisani
hapo, baada ya mazungumzo marefu waliagiza mwili wa marehemu urejeshwe na
kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ili usiharibike,” alieleza.
Aliongeza Polisi walishuhudia mwili
wa marehemu ukiwa umewekwa madhabahuni ;huku waumini wakiupapasa, wakiomba
afufuke.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo,
walisema Mchungaji Lwitiko aliwaongoza kwa mara nyingine kuurejesha mwili wa
marehemu ili uhifadhiwe chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Rukwa mjini hapa huku wakisisitiza kuwa maombezi yaliyofanyika kanisani hapo
ni ya imani yao.
Majirani walieleza umati mkubwa
ulifurika katika uwanja wa kanisa hilo, baada ya taarifa kuzagaa kuna marehemu
anaombewa mwili wake ukiwa madhabahuni, wakiamini atafufuka.
“Lakini walioruhusiwa kuingia
kanisani kwa maombezi, lazima awe muumini wa kanisa hilo na baada ya kuingia
mlango wa kanisa ulikuwa ukifungwa, “ alieleza mmoja wa waumini. Mwandishi wa
habari hizi alifika kanisani hapo jana asubuhi na kukuta milango imefungwa
;huku nyimbo zikiendelea kuimbwa kanisani.
Baadaye aliambatana na Mwenyekiti
Mwazembe na mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten kuingia kanisani kwa
mahojiano na mchungaji, lakini ndugu wa marehemu nusura wawapige, wakidai
hawakukaribishwa msibani.
“Kwanza nyie nani... mmekuja
kufanya nini hapa... ondokeni mara moja ....vinginevyo nendeni hospitali
mkaulize uzembe walioufanya na kusababisha kifo chake,” alifoka mmoja wa
wanandugu akitishia kuwapiga.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga
ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Dk Halfany Haule
alisema anafuatilia tukio hilo na atatoa taarifa baadaye.
Taarifa kutoka kanisani hapo,
zilieleza msiba huo upo Kitongoji cha Bangwe mjini Sumbawanga.
IMEANDIKWA NA PETI SIYAME, SUMBAWANGA.



