Wanajeshi FEKI Wawili Wakamatwa Dar

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kutumia sare za Jeshi la
Wananchi nchini (JWTZ) kufanya matukio mbali mbali ya kihalifu.
Wakati akizungumza na wanahabari jana
Disemba 22, 2017 jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, SACP Lazaro
Mambosasa, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Lainon Fratenus (20) na Noel
Cleophace Wagesa (30) wote wakazi wa Kigogo.

“Jeshi la Polisi mnamo Disemba 15,
2017 majira ya saa sita usiku maeneo ya Lugalo Kawe polisi wakiwa dolia
walifanikiwa kukamata wahalifu wawili wakiwa wamevalia sare za JWTZ na kisu
kimoja huku wakitumia gari namba T 306 CRU Toyota Carina rangi ya fedha,
wanatuhumiwa wanasadikiwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya uporaji jijini
Dar es Salaam,” amesema.
SACP Mambosasa amesema watuhumiwa
wanaendelea kuhojiwa ili kubaini mtandao mzima na matukio yote waliyowahi
kufanya na baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa watapelekwa mahakamani kwa
hatua zaidi za kisheria.




