Ukisikia Kakobe Akaongea, Tafakari Kwanza Kabla Ya Kumkabili- Askofu Kakobe

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel
Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amejibu hoja zinazotolewa dhidi yake,
baadhi zikitolewa na Serikali akisema anapozungumza ni lazima kutafakari kabla
ya kumkabili.
Askofu Kakobe alizungumza jana wakati
wa ibada katika kanisa la FGBF lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
“Ukisikia Kakobe amezungumza,
tafakari kwanza kabla ya kumkabili,” alisema.
Kauli hiyo aliitoa ikiwa ni siku moja
baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutangaza kuanza kufuatilia ulipaji
wake wa kodi.
Uamuzi wa TRAulitangazwa juzi na
Kamishna Mkuu, Charles Kichere mbele ya waandishi wa habari baada ya hivi
karibuni Askofu Kakobe kusikika akisema ana fedha nyingi kuliko Serikali.
TRA ilisema uamuzi huo unatokana na
kiongozi huyo wa kiroho kutokuwemo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za mamlaka
hiyo. Mamlaka hiyo ilisema kama utajiri wake unatokana na sadaka pekee litakuwa
jambo la kushtua.
Jana, Askofu Kakobe alitumia ibada
hiyo kuwajibu TRA na pia alizungumzia mambo mengine mawili; uraia wake na onyo
la Serikali la kuwataka viongozi wa dini kutokuzungumzia masuala ya siasa.
“Tangu nilipoitika wito huu miaka 30
iliyopita, sijawahi kufanya biashara yoyote zaidi ya hii na kanisa hili halina
mradi wowote wa kiuchumi. Kakobe hana mradi wowote na kama yupo anayejua
ajitokeze aseme nitampa zawadi,” alisema Askofu Kakobe.
“Akaunti yetu iko Benki ya NBC na iko
chini ya Bodi ya Wadhamini, bodi ambayo imesajiliwa Rita (Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini). Kwa hiyo, hao wanaotaka kujua zaidi waende Rita wakaulize
wajumbe wa bodi hii ni akina nani na waende NBC kuona vyanzo vyetu vya mapato
kama ni tofauti na sadaka.”
Huku akishangiliwa na waumini,
alisema tatizo kubwa lililojitokeza nchini ni watu kutafasiri wanavyojua na
kujikuta wakipotoka. Alisema hilo ni tatizo watu kutopenda kusoma Biblia kwa
undani na kwa upana zaidi.
“Wamemsikia Kakobe anazungumza hapa,
anazungumza mambo ya rohoni kuhusu haya ya utajiri. Unaweza kusikia maneno
ukatafsiri kivyako kwa sababu haya tunayozungumza hapa ni mambo ya rohoni, wewe
unayatafsiri kisiasa,” alisema Kakobe.
“Wanasema wewe una hela kweli kuliko
Tanzania sema... ninaweza kuvunja hekalu na kulisimamisha kwa siku tatu. Mtu
anajiuliza hekalu gani hili? Hekalu hili ni mwili wake. Maana yake niueni,
nisulubisheni, lakini nitakufa na siku ya tatu nitafufuka, hii ndio hekalu,
unatafsiri kwa akili.”
Kwa sauti ya juu na yenye msisitizo,
Askofu Kakobe alisema: “Kimsingi, mimi si mtu tu tajiri kuliko Serikali, bali
ni tajiri kuliko Serikali zote duniani. Kwa hiyo ukisikia Kakobe amezungumza,
tafakari kwanza kabla ya kumkabili.”
“Hela yote ya Serikali ya Tanzania au
dunia nzima haiwezi kununua tiketi hata moja ya Mbinguni. Mimi ni tajiri kuliko
Serikali ya Magufuli (Rais John Magufuli) au Serikali ya Trump (Rais wa
Marekani Donald Trump),” alisema.
Alisema nyumba anayoishi iliyopo Kijitonyama
karibu na Kituo cha Polisi Mabatini jijini Dar es Salaam aliijenga miaka ya
sabini na tangu wakati huo hajawahi kujenga kokote na gari lake ni la kawaida.
Askofu Kakobe alisema maisha yake si
ya kifahari kama wasemavyo watu.
Uraia wake:
Kuhusu uraia, Askofu Kakobe alisema
wazazi wake walikuwa wakiishi Kakonko mkoani Kigoma na baada ya kufariki
walizikwa huko, huku uraia wake ukifuatiliwa na ilibainika ni raia halali.
“Baba yangu alikuwa mwalimu kwa
kipindi kirefu, amefanya kazi Tanga, Sumbawanga, Usukumani kwa Wanyamwezi,
Tabora na Shinyanga. Miongoni mwa watu tuliocheza pamoja katika utoto wetu ni
Christopher Chiza, huyu alikuwa waziri,” alisema Kakobe.
“Ukitaja kwa jumla familia yetu,
inajulikana miaka mingi. Walikwenda kuchunguza uraia wangu na kujiridhisha
pasina shaka na kusema huyu ni Mtanzania. Kuna kipindi watu walikwenda mara
tatu kijijini kwangu Kakonko kuchunguza uraia.”
Waumini wakiwa kimya wakimsikiliza,
Askofu Kakobe alisema, ‘’ Nimezaliwa Tanzania, wazazi wangu wamezaliwa
Tanzania, mimi ni Mtanzania kwa hiyo sitoki hapa, tutabanana hapa hana.”
“Baada ya kuona, yote hayo, mara
waende huku, waende huko waulize wazazi wangu ambao wamefariki hivi karibuni na
makaburi yapo kijijini na niliwaambia makaburi wayaweke barabarani ili
anayechunguza uraia wangu aanzie pale,” alisema.
Alisema, ‘’Kila jambo chini ya mbingu
kuna kusudi, kuna kusudi la Mungu mimi kuzaliwa Tanzania, kwa hiyo wanaosema
nimetoroka hawanisumbui kichwa.”
Kuhusu taarifa za kutoroka nchini alisema:
“Ninapokwenda na kurudi washirika wa hapa wanajua. Kwa mfano safari ya mwisho
ilikuwa Agosti (mwaka jana) na tangu hapo sijasafiri. Niko hapa na haya mengine
nayasikia nimetoroka, hayanisumbui, ukiitwa majina si yako unasumbukia nini?”



