Askofu Kakobe Amuomba Radhi Jpm Kauli Ya "Ana Fedha Kuliko Serikali"

ASKOFU wa Kanisa la Full Gospel Bible
Fellowship, Zachary Kakobe amemuomba radhi Rais John Magufuli kutokana na kauli
yake kuwa yeye (Kakobe) ana fedha kuliko Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Charles Kichere amesema leo jijini Dar es Salaam kuwa, Januari
24 mwaka huu, Askofu Kakobe aliandika barua kwa Rais Magufuli kuomba radhi.
Amesema, TRA imechunguza kauli ya
Kakobe na kubaini kuwa hana akaunti wala fedha kwenye taasisi yoyote ya fedha
nchini.
Kichere amesema, uchunguzi huo
umebaini kuwa, Kakobe ni mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti ya kanisa hilo
iliyopo Benki ya NBC.
Kwa mujibu wa Kichere, akaunti hiyo
ina shilingi 8,132,100,819.00 zilizotokana na sadaka, zaka, na michango ya
waumini na kwamba, kwa mujibu wa sheria, fedha hizo hazitozwi kodi.
“Aidha, wakati uchunguzi huo
ukiendelea, mnamo tarehe 24.01.2018 Askofu Kakobe aliandika barua kwa
Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuomba radhi kutokana na
kauli yake ya kebehi pamoja na matamshi yake ya dharau kwamba, ana pesa nyingi
kuliko serikali” amesema Kichere.
NA BASIL MSONGO -
HABARILEO



