Sakata La Uanachama Wa Zanzibar Fifa, Wabunge Wa CUF Wamwandikia Barua Rais Wa FIFA
Wabunge
wa Chama cha Wananchi (CUF), wamemuandikia barua ya wazi Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) Gianni Infantino, kumwelezea kilio cha Wazanzibar
kuhitaji haki yao ya Zanzibar kuwa mwanachama FIFA.
Pia wamesema watafungua shauri mahakamani ili kutafuta uhalali wa
kikatiba wa chombo cha Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kufanya kazi
ya muungano na iizuie TFF kufanya kazi yoyote mpaka uamuzi utakapotolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mnadhimu
wa Kambi ya CUF Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Malindi, Zanzibar Ally Saleh alisea wanapenda kuufahamisha
umma juu ya barua waliyoandika kwenda kwa rais huyo wa FIFA.
Alisema Sisi wabunge wa wananchi tunathamini juhudi zinazochukuliwa na kuipigania Zanzibar, lakini kuna msemo wa Kiswahili unaeleza ukibebwa ujikaze na pia mwengine unaosema mshike mshike na mwenyewe uko nyuma.
“Kwa sababu hiyo basi pamoja na mazungumzo ambayo yatafanywa
kuendelea kuishawishi FIFA ielewe hali ya Zanzibar basi na sisi tumeona pia
tupaze sauti zetu hasa kwa sababu viongozi wa FIFA wapo nchini lakini zaidi kwa
sababu rais wa taasisi hiyo yupo nchini, hivyo tumemwandikia barua ya wazi,”
amesema na kuongeza Saleh.
Mhe. Saleh aliongeza kuwa kapitia barua hiyo wamemweleza mambo SITA,
mambo hayo ni TFF haiwakilishi maslahi ya Zanzibar, mamlaka ya TFF haijawahi
wala hayafiki Zanzibar, muundo wa TFF ni kuwa na vyama vya mikoa, wakati ZFA
ina mikoa yake.
Alitaja Mengine ni TFF haijawahi kuwa na sera ya maendeleo
inayohusisha Zanzibar, TFF inasimamia Kilimanjaro Stars na kuifanya timu ya
Taifa Stars na mwisho hakuna kikao chochote cha kikatiba baina ya TFF na ZFA.
Aidha Mhe. Saleh alibainisha kuwa pamoja na kwenda mahakamani
kutafuta uhalali wa TFF kufanya kazi ya muungano, ametaja mambo mengine
watakayotaka kupatiwa ufafanuzi na mahakama ili waweze kufanikiwa kupata haki
yao ya uanachama wa FIFA.
Ametaja kuwa ni kuitaka mahakama iwape muongozo juu ya kwa nini
pasiwepo chama cha soka cha Tanzania Bara na kutafuta tafsiri ya waziri wa
michezo wa Tanzania Bara kutumika kama ni waziri wa muungano ndani na nje ya
nchi.
Pamoja na hayo amebeinisha kuwa watatoa hoja binafsi bungeni
kuhusu mustakabali ya michezo chini ya utaratibu tata uliopo hivi sasa.
“Tunaamini bila kufanya hatua hiyo hapatakuwa na suluhu kwa sababu
hali hii imeendelea kwa muda mrefu na tumekuwa tukijificha kama mbuni kufanya
kana kwamba sababu ya Zanzibar kukosa uanachama wa FIFA haitokani na muungano
na muundo wake,” ameeleza Saleh.




