Lowassa Awapongeza Maaskofu...Ataka Kinondoni Wasilale Mpaka Kieleweke

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na
Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amewapongeza maaskofu kwa kuunga mkono
mambo aliyosema wamekuwa wakiyapigania.
Lowassa ametoa pongezi hizo jana
Februari 11,2018 akimnadi mgombea ubunge jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu
katika Kata ya Kijitonyama.
“Leo kwenye magazeti wameandika
kwamba Baraza la Maaskofu wamezungumzia mambo ambayo tumekuwa tunayasema kila
siku, kuhusu kuzuia uhuru wa kuzungumza na suala la maadili. Ninawashukuru sana
maaskofu, ninawapongeza sana kwa kuunga mkono ambayo tumekuwa tunayasema,”
amesema Lowassa.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC), limetoa ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2018 ndani yake likitoa msimamo
kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.
Lowassa akimnadi Mwalimu alisema
anamfahamu kwamba ni kijana shupavu na mchapa kazi ambaye akipewa kura wananchi
wa Kinondoni watapata maendeleo.
“Kinondoni msilale mpaka kieleweke.
Mchagueni Salum Mwalimu akawaletee maendeleo,” amesema.
Mwalimu akiomba kura amesema
Kinondoni ni watu ambao wanajitambua.
“Kinondoni ni watu mnaojitambua, ni
watu ambao mlijitoa mwaka 2015, wengine waliachika. Ninawapenda sana, ninajua
nina deni kubwa la kuwalipa,” amesema.
Mwalimu amesema, “Ninapozungumza
najua ninazungumza na wajanja ambao hawadanganyiki. Tangu juzi, wenzangu
wameleta fedha hapa Kijitonyama kwa ajili ya kununua shahada.”
Amesema waliposikia anagombea ubunge
walipata hofu kubwa, vikao vikawa haviishi wakitafakari itakuwaje nikienda
bungeni.
Na Peter Elias, Mwananchi



