ACT Wazalendo kufungua Kesi Madai Dhidi Ya Jeshi La Polisi

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimefungua kesi ya
madai Na. 8/2018 mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam kulishtaki jeshi la polisi
ikidai jeshi hilo kuingilia visivyo halali shughuli za ziara za viongozi wa
chama hicho kwenye kata wanazoongoza.
Pia kimejipanga kupeleka bungeni mpango
mbadala juu ya sera za kibajeti za nchi kwa kupinga mpango wa sasa wa bajeti
unaojikita kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu.
Hayo yemesemwa leo jijini Dar es Salaam na
kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari kuelezea waliyobaini katika ziara za viongozi walizofanya katika kata
wanazoongoza kuanzia Febriari 19, 2018 hadi Machi 13, 2018.
“Ziara yetu kwenye kata tunazoongoza
ilibughudhiwa na vyombo vya dola. Jeshi la polisi na baadhi ya watendaji
wa serikali walihaha sana kuingilia na kujaribu kuikwamisha ziara yetu,”
amesema Zitto.
Ameongeza “Kilele cha jitihada hizi ni
kukamatwa na kulazwa kwangu rumande Mkoani Morogoro usiku wa kuamkia Februari
23, 2018 nikiwa katika kata ya Kikeo, Mvomero, Morogoro, kuzuiliwa kutembelea
miradi ya maendeleo kwenye kata za Vumilia-Urambo na Usinge-Kaliua mkoani
Tabora pamoja na kuzuiwa kabisa hata kufanya mkutano wa ndani na diwani wetu
katika kata ya Liale, Mvomero, mkoani Morogoro.”
Akizungumzia kuhusu kupeleka bungeni mpango
mbadala juu ya sera za kibajeti, Zitto amesema masuala watakayosimamia ni
uchumi shirikishi unaozalisha ajira kwa kuhakikisha kilimo pamoja na viwanda
vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo ndio kipaumbele kikuu,
usalama wa chakula na lishe, pamoja na huduma bora za kijamii, hasa maji, elimu
na Afya.
Waliyobaini katika
ziara
Kiongozi huyo ambaye pia ni mbunge wa Kigoma
Mjini, amesema katika ziara hiyo imewaonyesha kuwa hali ya maisha ya
wananchi vijijini ni mbaya sana.
Amesema katika kata zote walizotembelea
wamekuta tatizo kubwa ni hali mbaya ya kipato, migogoro ya ardhi,
kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama, ukosefu wa huduma bora za afya,
tatizo la miundombinu ya usafirishaji, ukosefu wa pembejeo za kilimo na ukosefu
wa masoko ya mazao ya wavuvi, wakulima na wafugaji pamoja na kushuka kwa bei ya
mazao yao.
Mengine ni kupanda kwa gharama ya maisha ya
watu, kupanda kwa gharama ya vifaa vya ujenzi, upungufu mkubwa wa vyumba vya
madarasa, vyoo pamoja walimu na kuzorota kwa hali ya usalama wa wananchi pamoja
mali zao, hali mbaya ya ajira kwa vijana pamoja na uminywaji mkubwa demokrasia
na uhuru wa vyobo vya habari.
Pia Zitto ameendelea kuweka msisitizo uwepo wa
mkutano wa maridhiano wa kuona ni namna gani shughuli za kisiasa zinaweza
kufanyika nchini kwa ajili ya maendeleo ya taifa.



