Askofu Shoo Kanisa Halitakubali Kuzibwa Mdomo… Aeleza Maaskofu KKKT Walivyofunga Kabla ya Kutoa Waraka

Askofu Mkuu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo ameonya
kwamba asitokee kiongozi yeyote nchini wa kisiasa au serikali ambaye atajaribu
kuwazuia na kuwaziba midomo viongozi wa dini kutekeleza wajibu wao wa kukemea
na kuonya juu ya maovu yanayoendelea hapa nchini.
Dk. Shoo ambaye
pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, pia amesema kamwe kanisa halitanyamaza
kimya kwa wanasiasa wenye tabia ya kutumia nafasi zao kuligawa taifa vipande
vipande.
Alizungumza
hayo jana kwenye ibada maalumu ya kusataafu kwa aliyekuwa Mchungaji wa
Usharika wa Masama Kati, John Mshau wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
“Wajibu wa viongozi wa dini ni kuonya na kukemea yale mabaya
yanayoendelea nchini na si vinginevyo na kwamba asijaribu kutokea mtu
yeyote kuwazuia viongozi wa dini kufanya wajibu huo kwani ni sawa na kupingana
na Mungu.
“Wajibu wetu ni kuonya, kushauri, kukemea na tunatenda hivyo, asijaribu
kuja mtu yeyote kutuzuia kufanya hivyo kwani neno la Mungu linasema bwana
hutegemeza wenye upole na huangusha chini wenye hila, hivyo sisi kama viongozi
wa dini hatutakubali kunyamaza tutasema na kukemea maovu,” amesema
Pamoja na mambo
mengine, Dk. Shoo aliwaonya viongozi wote wa kisiasa nchini kuacha kutumia
vyama vyao kuligawa taifa na kwamba suala hilo halitaweza kuvumiliwa na
viongozi wa dini na wataendelea kusema na kuonya.
Akitolea ufafanuzi
waraka ulioandaliwa na Baraza la Maaskofu 27 wa KKKT, Machi 15 Jijini Arusha
alisema walifunga na kuomba Mungu kwa lengo la kupata ujumbe sahihi ili wautoe
kwa waumini wa kanisa hilo na Taifa kwa ujumla na kwamba hawakukurupuka kutoa
ujumbe huo.



