Baraza La Wakunga Latoa Tamko Kufatia Kuripotiwa Wauguzi Kupigwa Na Kuwekwa Rumande
Baraza la
Uuguzi na Ukunga Tanzania limelaani hatua zilizochukuliwa na baadhi ya viongozi
kwa wauguzi.
Katika
tamko la baraza hilo, limelaani tukio la Machi 7,2018 katika Hospitali ya Wilaya
ya Tandahimba mkoani Mtwara ambalo muuguzi Amina Nicodemus aliwekwa ndani kwa
amri ya mkuu wa wilaya akituhumiwa kuuza nguo za watoto akiwa kazini.
Tukio
lingine ni la Machi 8,2018 lililotokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga ambako muuguzi Hilda Ebunka alipigwa na diwani akiwa kazini.
Katika
tamko lililotolewa jana Jumapili Machi 11,2018 na Msajili wa Baraza la Uuguzi
na Ukunga Tanzania, Bi Lena Mfalila limeeleza vitendo hivyo ni udhalilishaji na
ni kinyume cha miongozo ya kisheria inayosimamia ushughulikiaji wa tuhuma za
uvunjifu wa nidhamu na sheria wakati wa kazi.
"Kumpiga
mtumishi wakati akiwa kazini ni udhalilishaji na ni kinyume cha sheria. Nidhamu
ya wauguzi na wakunga inasimamiwa na sheria inayotoa mamlaka ya kuchukua hatua
za kinidhamu kwa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania," amesema Mfalila.
Viongozi
wa kitaifa, wakiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais – Tamisemi, Selemani Jafo; na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa nyakati
tofauti wamekemea matukio hayo.
"Kwa
tamko hili baraza linalaani vitendo vilivyofanywa na viongozi husika na linatoa
pole kwa wauguzi waliopatwa na kadhia hii," amesema Mfalila.




