Kauli Ya LISSU Ujio Wa Bombardier Iliyokuwa Imezuiliwa Canada.
Mbunge wa Singida, Tundu Lissu
amesema ameona taarifa ya Msemaji wa Ikulu, Gerson Msigwa, kwamba ndege aina
Bombardier iliyokuwa imezuiliwa Canada inakuja nchini.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram
Lissu ameandika baadhi ya mambo ambayo angependa baadhi ya watu wanaodai kuwa
alitumwa kipindi cha nyuma alipokuwa anazungumzia kushikiliwa kwa ndege hiyo
Canada wafahamu.
Jambo la kwanza alilolisema Lissu
katika ukurasa wake wa Instagrama ni kuhusu kuvunjwa kwa mkataba uliosababisha
ndege kuzuiliwa “Mwaka 2003, kampuni ya Sterling Construction and Engineering
Ltd. (SCEL), ilivunjiwa mkataba wake wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo. Mkataba
huo ulivunjwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.”
“Baada ya kuvunjwa kwa mkataba, SCEL
ilishtaki Serikali ya Tanzania kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya International
Chamber of Commerce, London. Tunaambiwa baadhi ya hearings, au zote,
zilifanyikia Dar Es Salaam.” -Lissu
Jambo la pili aliloliandika Lissu ni
kuhusu serikali kuamriwa kulipa kampuni “December 2009 na baadae June 2010,
Arbitral Tribunal ya ICC ilitoa uamuzi kwamba Serikali ya Tanzania ilivunja
mkataba wa SCEL bila uhalali wowote na kuamuru Serikali kuilipa SCEL takriban
USD milioni 25, na riba ya 8% kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu hadi tarehe ya
malipo ya mwisho.”
“Kwa sababu tunazostahili kuambiwa na
Serikali , deni la SCEL halikulipwa kwa miaka saba hadi SCEL walipoenda kwenye
Supreme Court of Quebec, Canada, na kupata amri ya mahakama kuikamata
Bombardier.” -Lissu
Lissu akaendelea kuandika kwamba
baada ya kusikia Bombardier imekamatwa, Waziri wa Mambo ya Nje, Dr. Augustine
Mahiga, na Balozi wetu Canada, Jack Zoka, walitumwa kwenda Toronto kufanya
mazungumzo na SCEL juu ya namna ya kujinasua. Waziri Mahiga na Balozi Zoka
waliiomba SCEL isitoe habari za Bombardier kukamatwa hadharani.
“August 18, 2017, baada ya kupata
nyaraka mbali mbali zinazohusu kukamatwa kwa Bombardier, nilitoa taarifa za
kukamatwa ndege hiyo kwa waandishi wa habari Courtyard Hotel, Dar Es Salaam.”
-Lissu
“August 19, Kaimu Msemaji wa Serikali,
Zamaradi Kawawa, alithibitisha kukamatwa kwa Bombardier ya Magufuli na
kutulaumu sisi wapinzani kuwa ndio tuliosababisha ndege yetu ikamatwe Canada.”
-Lissu
“Licha ya Serikali kukiri ukweli wa
maneno yangu, tarehe 20 August, nilikamatwa na askari polisi walioniambia
hawajui kosa langu ila wanatekeleza ‘maagizo.’ Nililazwa mahabusu hadi kesho
yake nilipopelekwa kwa Mkemia Mkuu ili kupimwa mkojo. Nilipokataa kupimwa mkojo
nilirudishwa mahabusu hadi kesho yake tarehe 22 August nilipoachiliwa huru bila
kupelekwa mahakamani.” -Lissu
“September 7, 2017, siku kumi na moja
baada ya shambulio la mabomu dhidi ya IMMA Advocates, ikawa zamu yangu
kushambuliwa kwa risasi za submachine guns na ‘watu wasiojulikana.’
Nilijeruhiwa vibaya sana, lakini Mungu ni mwema sikufa. Hadi ninapoandika
maneno haya, hakuna mtu hata mmoja aliyetuhumiwa au kukamatwa na kushtakiwa kwa
kuhusika na shambulio hilo la kigaidi dhidi yangu.” –Lissu
Lissu akamaliza kwa kusema “Nafurahi
kusikia taarifa za kuachiliwa kwa ndege yetu. Nitafurahi zaidi tukiambiwa
Bombardier hiyo imeachiliwa kwa masharti gani, kwa vile tulikuwa tunadaiwa
karibu USD milioni 40 zilizotokana na kuvunja mkataba na Serikali kushindwa
kesi na SCEL. Hili ni swali ambalo kila mmoja wetu anatakiwa kuwahoji hawa
watoa taarifa za kuachiliwa kwa Bombardier.”



