Rais Ajiuzulu…Waziri Mkuu Atoa Taarifa

Rais wa Mauritius, Ameenah Gurib-Fakim
amelazimika kujiuzulu baada ya kuandamwa na kashfa ya fedha.
Taarifa
za kujiuzulu kwake zimetangazwa leo Machi 10, 2018 na Waziri Mkuu wa nchi hiyo,
Pravind Jugnauth.
Gurib-Fakim,
ambaye ni rais pekee mwanamke barani Afrika ameshutumiwa kwa kutumia kadi ya
benki iliyotolewa na shirika moja lisilo la kiserikali kwa ajili ya matumizi
yake binafsi.
Atajiuzulu
wadhifa huo Machi 12, 2018 wakati Taifa hilo litakapoadhimisha miaka 50 ya
uhuru.
"Rais wa Jamhuri ameniambia kuwa anajiuzulu na tumekubaliana tarehe ya
kuondoka,” amesema Jugnauth wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
mjini Port Louis.
Katika
miezi ya hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya marais barani Afrika
kuachia madaraka kwa kushurutishwa au kujiuzulu kwa hiari.
Miongoni
mwa mataifa yaliyoshuhudiwa hali hiyo ni pamoja na Afrika Kusini, Zimbabwe na
Ethiopia.
Rais huyo
wa Mauritius aliingia madarakani mwaka 2015 kama rais wa heshima na kuwa
mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika Taifa hilo.
Amekuwa
akiandamwa na shinikizo kali tangu gazeti la L'Express lilipochapisha taarifa
zilizoeleza jinsi taasisi moja ya Uingereza ilivyompatia kadi ya benki
iliyomwezesha kufanya manunuzi ya hali ya juu katika maduka mbalimbali.
Taasisi
hiyo ya Planet Earth Institute imekuwa ikidhaminiwa na bilionea wa Angola
,Alvaro Sobrinho ambaye anachunguzwa kutokana na kashfa mbalimbali ikiwamo
utakatishaji wa fedha.



