Kutoka Shinyanga: Diwani Ampa Kichapo Nesi Mbele Ya Wagonjwa

Wakati wanawake wakisherekea siku ya
wanawake duniani, Nesi aliyejulikana kwa jina moja la Hilda akiendelea kuhudumia
wagonjwa katika kituo cha afya cha Bunambiyu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
amejikuta katika wakati mgumu baada ya kushambuliwa kwa kuchapwa vibao na
diwani wa kata ya Bunambiyu Richard Sangi Sangi (CCM).
Inaelezwa kuwa chanzo cha tukio
hilo lililotokea leo Alhamis Machi 8,2018 majira ya saa tatu na nusu
asubuhi, ni diwani huyo kumtuhumu nesi huyo kuwa hahudumii wagonjwa vizuri
na kumtaka aondoke kituoni na alipogoma ndipo diwani alipoamua kumshambulia
nesi huyo mbele ya wagonjwa.
Diwani
huyo alipigiwa simu na wananchi wakimwelezea kuwa mgonjwa wao aliyelazwa katika
kituo hicho cha afya kwa zaidi ya wiki moja hapatiwi huduma vizuri na ndipo
diwani huyo alipoomba kuongea kwa simu na nesi aliyepo zamu,nesi akamsihi
diwani afike ofisini/kituoni na alipofika akaanza kumshambulia nesi huyo.
“Huyu diwani amekuwa kama
rais, wananchi wanapeleka malalamiko yote kwake, alipigiwa simu kuwa mgonjwa wao
hapatiwi huduma vizuri hali inayosababisha aendelee kulazwa”, kilieleza chanzo
cha habari cha Malunde1 blog.
Hata hivyo habari zaidi
zinasema,wakati nesi Hilda akiendelea kuhudumia wagonjwa, ghafla nesi mwingine
ambaye hakuwa zamu aliingia katika wodi ya wagonjwa na kuwaambia ndugu wa
mgonjwa huyo kuwa ndugu yao ana upungufu wa damu hivyo anatakiwa kupewa rufaa
kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
“Kutokana na hali hiyo ndipo ndugu wa
mgonjwa wakaamua kumpigia simu diwani na kutaka kuongea kwa simu na nesi wa
zamu,nesi akaomba diwani afike ofisini,alipofika ndipo akaanza kuonesha ubabe
kwa kumshambulia nesi ambaye alikuwa zamu na alikuwa anasimamia kituo cha afya
kutokana na mganga mkuu wa kituo kutokuwepo kazini”,kilieleza chanzo
chetu.
Taarifa ambazo mtandao huu umezipata
ni kwamba tayari nesi huyo ameelekea kituo cha polisi kutokana na tukio hilo la
kushambuliwa na kudhalilishwa na diwani huyo.
Kaimu Mkuu wa wilaya ya
Kishapu, Josephine Matiro amesema tayari amepokea taarifa za tukio hilo na
anazifanyia kazi.
Source Malunde 1



