Raisi Mstaafu Kikwete Mgeni Rasmi Harambee Ya Kukusanya Bil 1 Za Ujenzi Wa Shule Ya Sekondari Iliyoungua Mkoani Lindi.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi
Na Jemsi Kandoya
RAISI Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
harambee ya kukusanya fedha kiasi cha Sh. bilioni moja kwa
ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Lindi iliyoungua Julai 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu
wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, alisema harambee hiyo itafanyika Machi
29 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Zambi alisema maandalizi yote kwa ajili ya harambee hiyo
yamekamilika na inatarajia kuhudhuriwa na wadau wengine wa sekta ya elimu
nchini.
Alisema harambee hiyo imepanga kukusanya Sh. bilioni moja ikiwa ni
karibu nusu ya mahitaji ya Sh. bilioni 2. zinazotakiwa kwa ajili ya ujenzi wa
shule hiyo kongwe.
“Ni matumaini yetu kuwa kutokana na fedha tutakazokusanya,
tumepanga ujenzi uanze wakati wowote. Zoezi hili litakwenda sambamba na mpango
wa mkoa kuboresha mfumo mzima wa masuala ya elimu toka ngazi ya awali,” alisema
Zambi.
Mkuu wa Mkoa huyo alikiri kuwa mkoa wake ni mmoja kati ya
inayofanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani, akieleza kuwa hatua madhubuti
zimechukuliwa ikiwamo kupima uwezo wa walimu.
Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Emmy Mchuchuri, alitaja
changamoto zinazoukabili mkoa huo katika kutoa elimu ikiwamo miundombinu
mibovu, uzembe wa walimu, utoro na kutokuwapo kwa chakula shuleni.
Alisema kuwa ofisi yake imeanza kutekeleza maadhimio ya wadau juu
ya namna bora ya kuboresha elimu ndani ya mkoa huo ikiwamo utoaji wa chakula
cha mchana mashuleni, mafunzo kwa walimu ili kujenga uwezo wao wa ufundishaji.
Alibainisha kuwa sambamba za zoezi hilo, walimu watakaobanika kuwa
na viwango vidodgo vya ufundishaji watashushwa madaraja yao.



