Diamond Akutana Na Waziri Mwakyembe Na Shonza
Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe leo Jumanne Machi
27, 2018 amekutana na mwanamuziki Nassib Abdul maarufu Diamond Platnumz, jijini
Dar es Salaam.
Tarifa
iliyotolewa leo na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Lorietha
Laurence imesema lengo la kukutana kwa wawili hao ni kurejesha maelewano kwenye
tasnia ya muziki kufuatia hatua zinazochukuliwa na wizara hiyo kufungia baadhi
ya nyimbo, zikiwemo mbili za mwanamuziki huyo.
Imeeleza
kuwa katika kikao hicho kilichofanyika ofisi za wizara hiyo na kuchukua zaidi
ya saa tatu, kilihudhuriwa na naibu waziri wa wizara hiyo, Juliana Shonza,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mwingereza.
Wengine
ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisoo huku Diamond
akifuata na mameneja wake watatu, Sallam Sharaff, Hamis Taletale na Said Fela.
Taarifa
hiyo inaeleza mazungumzo hayo, Diamond alimhakikishia Dk Mwakyembe kushirikiana
kwa karibu na Shonza na uongozi mzima wa wizara katika kusimamia maadili ya
kazi za sanaa na kuwa mfano bora wa wasanii nchini katika kulinda utamaduni wa
Tanzania.
Kwa
upande wake Dk Mwakyembe amesisitiza kuwa Serikali haina ugomvi wowote na
wasanii nchini bali ina tatizo na mmomonyoko wa maadili, kwamba kila msanii ana
wajibu kulinda maadili ambayo ni sehemu ya utamaduni wa nchi.
“Mwakyembe
alikumbushia kauli ya Mwalimu Julius Nyerere baada ya uhuru kwamba Taifa lisilo
na utamaduni wake ni sawa na Taifa mfu na Watanzania kamwe tusigeuke Taifa
mfu,” inaeleza taarifa hiyo ikimnukuu Dk Mwakyembe.
Waziri
huyo ameagiza watendaji wa wizara na taasisi zake ikiwemo Basata, Bodi ya
filamu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kukutana na makundi ya
wasanii wa muziki kwa lengo la kuelimishana kuhusu taratibu za kuwasiliana na
mamlaka husika za sanaa.
"Maamuzi
ya kuzifungia baadhi ya nyimbo yanayafanywa kwa mujibu wa sheria na si kwa
utashi binafsi wa kiongozi wa wizara. Hivyo basi ieleweke kwamba hatua
zilizochukuliwa na Shonza hivi karibuni zilikuwa za wizara kwa mujibu wa sheria
za nchi,” amesema Dk Mwakyembe.
Kwa
upande wake Shonza amesisitiza umuhimu wa wasanii kufuata utaratibu kwa
kuwasilisha kazi zao mapema kwenye mamlaka husika iii kuepusha matatizo
baadaye.
Lorietha
Laurence Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo. 27/03/2018.



