CHADEMA Yanusha Habari Ya Tundu Lissu Kuwasili Muda Wowote

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
kimekanusha taarifa zinazoendelea mitandaoni kuhusu uwezekano wa kurejea nchini
kwa Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu kutokea Ubelgiji alipokuwa
akipatiwa matibabu tangu mapema Januari mwaka huu.
Kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari
na Mawasiliano CHADEMA, Ndg. Tumaini Makene amesema kwamba kupitia mitandaoni
mapema leo kumekuwa na taarifa za kwamba Lissu anatarajiwa kurejea nyumbani
Tanzania wakati wowote kuanzia juzi, kwamba amemaliza matibabu yake kitu ambacho
sicho cha kweli na kimezua taharuki.
Katika taarifa yake Ndg. Makene
amesema kwamba Mwanasheria huyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki,
hajazungumza na mwandishi wa habari yeyote juu ya kurejea kwake nyumbani kwa
sababu zilizo wazi kabisa kuwa bado hajapona na anatarajiwa kufanyiwa upasuaji
mwingine mwisho wiki hii au wiki ijayo.
Hata hivyo chama hicho kimetoa wito
kwa na wanachama na Watanzania wote wenye mapenzi mema kutokana na kuguswa na
uzito wa masahibu yaliyompata Lissu wameendelea kuguswa na kufuatilia kwa
ukaribu maendeleo ya matibabu na hali ya afya yake kupuuza taarifa hizo.
Tundu Lissu yupo nchini Ubelgiji
akipatiwa awamu ya tatu ya matibabu baada ya kumaliza matibabu nchini Kenya
mwezi Januari ambapo alikuwepo huko kwa takribani miezi minne ambapo alikuwa
akiuguza majeraha ya risasi.
Mbunge huyo machachari alipigwa
risasi zilizokadiriwa 37 nje ya makazi yake huko Jijini Dodoma majira ya saa 7
mchana na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akitoka kwenye majukumu yake ya
kibunge.



