Profesa Jay Akumbuka Msoto....Asimulia Alivyokuwa Anakunywa Maji Ya Chooni Na Kupanda Malori

Nguli wa muziki wa Bongo Fleva ambaye
pia ni mbunge wa jimbo la Mikumi, Joseph ‘Profesa Jay’ Haule, amekumbuka msoto
aliokutana nao wakati anatafuta kutoka kimuziki miaka ya 1990 akiwa na Hard
Blasters Crew (HBC).
Akifunguka kupitia The Playlist ya
Times FM, rapa huyo mkongwe aliyechonga barabara kwa wasanii wengi wa rap
nchini, amesema kuwa wakati wanaandaa albam zao na HBC, hawakuwa na kitu
mfukoni kiasi cha kufikia hatua ya kunywa maji ya bomba lililokuwa chooni ili
waendelee kufanya kazi yao studio.
“Nakumbuka wakati huo tunarekodi,
unaenda kunywa maji chooni hivi… kwenye bomba liliko chooni unakula na mihogo
yako ili uweze ku -buy time ya kuendelea kuwa studio siku nzima. Kwamba hakuna
hata pesa ya kula chips mzee,” Profesa alifunguka.
Mkali huyo wa rap mwenye majina mengi
ya kupewa kwa kuwa mbabe wa kurap, alieleza kuwa wakati wamepata nafasi ya
kurekodi albam yao kama HBC, kuna wakati akiwa anafanya kazi Tanga, ilimlazimu
kupanda malori ya mizigo usiku ili arejee kazini Jumapili usiku, kwani muda wa
usiku aliokuwa akimaliza kurekodi jijini Dar es Salaam, magari ya abiria
hayakuwepo.
Katika hatua nyingine, Profesa Jay
alieleza tukio la kurekodi wimbo wake wa ‘Jina Langu’ katika studio za Bongo
Records chini ya mtayarishaji nguli, P-Funk Majani. Alisema alimshangaza Majani
kwani alikuwa akisikia mara kadhaa mdundo wa wimbo huo, ndipo alipomuomba
mtayarishaji huyo aingize sauti.
Alisema baada ya kuwekewa mdundo,
alipita na mashairi yote matatu bila kukwama, kitu ambacho kilimshangaza Majani
pamoja na ukubwa wa mashairi yaliyowekwa ndani.
Profesa amewashauri wasanii wa
Tanzania kuendelea kuandika vitu ambavyo vinagusa jamii na kuitangaza Tanzania
kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.
Hivi karibuni, aliachia wimbo wake
‘Pagamisa’ akiwa na mtayarishaji wa muziki, Mr. T-Touch.



