Waziri Kairuki Aagiza Bilioni 30 Sekta Ya Madini, Mafuta Zichunguzwe Zilipo

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
amezindua ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na malipo ya
kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16
iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini,
Gesi Asilia na Mafuta Tanzania (TEITI) kwa kushirikiana na Mtaalam
Mwelekezi, Boas & Associates na MM Attoneys.
Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti
hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha wawakilishi kutoka
Kamati ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi, Waziri Kairuki
amepongeza Kamati ya TEITI na Sekretarieti kwa mchango wake katika
uandaaji wa ripoti hiyo.
Mbali na Pongezi hizo, Kairuki
ameiagiza Kamati ya TEITI kuongeza nguvu katika kuhakikisha wananchi
wanakuwa na uelewa mpana wa umuhimu na wajibu wa TEITI kwa kutumia mbinu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na warsha mbalimbali pamoja na vipindi vya redio
na televisheni.
Amesisitiza kuwa, kipaumbele
kiwekwe kwenye maeneo yaliyozungukwa na shughuli za utafutaji na
uzalishaji wa madini, mafuta na gesi asilia na kupata taarifa ndani ya kipindi
cha miezi sita.
Awali akielezea ripoti hiyo,
Kairuki amesema kuwa ripoti hiyo inahusu tathmini ya mapato ya madini
katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2015 hadi tarehe 30 Juni, 2016 na
kufafanua kuwa jumla ya shilingi 434,627,874,380 zilipokelewa serikalini
kutoka kwenye kampuni 55 za madini, mafuta na gesi asilia zilizoshiriki zoezi
la ulinganishi.
Hata hiyo amesema taarifa inaonesha
kuwa kampuni zililipa kiasi cha shilingi 465,164,747,725 za kitanzania serikalini
na kusababisha tofauti kati ya malipo kuwa ni pungufu ya shilingi
30,536,873,345 za kitanzania chini ya kiasi ambacho Serikali imekiri kupokea.
“Ni lazima tufahamu ni vipi
imejitokeza tofauti hii na ninachukua fursa hii kuelekeza taarifa hii kupelekwa
kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajiili ya uchunguzi kama
kifungu 18(1) cha Sheria ya TEITI ya mwaka 2015 kinavyotaka,” alisema Waziri
Kairuki.
Katika hatua nyingine, Waziri
Kairuki amefafanua kuwa ripoti imeonesha kuwa sekta ya madini imechangia
zaidi kwa asilimia 85 na sekta ya mafuta na gesi ikionyesha kuchangia
asilimia 15 ya mapato ya Serikali chini ya Sekta ya Madini kwa mwaka 2015/16
Akielezea mafanikio ya Serikali ya
Awamu ya Tano katika sekta ya madini, Kairuki amesema kuwa ili kuhakikisha
madini yanakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, Serikali imeanza
kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya Sheria ya Madini
pamoja na kanuni zake.
Ametaja hatua nyingine ambayo ni
endelevu kuwa ni kufanya tathmini ya jinsi gani nchi inapata mapato yake
kwenye sekta ya madini kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa.
Ameendelea kusema kuwa jukumu
linafanywa na taasisi mbalimbali za Serikali lakini TEITI nayo
inatekeleza jukumu husika kwa kuhakikisha taarifa za mapato ya madini
zinatolewa kwa uwazi kwa wananchi na wadau mbalimbali katika Serikali,
Sekta Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Wakati huo huo akizungumza na
waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila
amesema kuwa mara baada ya ripoti kuzinduliwa na kukabidhiwa kwa Kamati ya
TEITI hatua inayofuatia ni kamati ya TEITI kuwasilisha ripoti hiyo kwa Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali ili achukue hatua kwenye hoja zilizotokana na ripoti
hiyo.
Profesa Msanjila amezitaka kampuni
nyingine ambazo hazikushiriki katika kipindi cha ukaguzi kujitokeza katika
ukaguzi unaofuata ili takwimu halisi za mapato zifahamike.
Aidha, ametumia fursa hiyo
kukaribisha kampuni nyingine zenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya madini
kujitokeza kwa wingi ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa katika
ukuaji wa uchumi.



