Askofu Wa Kanisa La KKKT Apigwa Mawe
ASKOFU wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika mkoani Rukwa
jana alifukuzwa kwa mawe baada ya baadhi ya waumini kumzuia kuingia usharikani
wakidai hawataki kumuona akiwepo eneo la kanisa.
Tukio hilo
ambalo lilishuhudiwa na mwandishi wa habari lilitokea saa 2:00 asubuhi katika
Usharika wa Sumbawanga Mjini, muda mfupi baada ya Askofu Ambele Mwaipopo
kufika.
Kumezuka
mgogoro baina ya waumini na uongozi wa dayosisi kufuatia mchungaji kiongozi
kipenzi cha washarika kuhamishwa.
Askofu Mwaipopo
alikuwa ameongozana na Mkuu wa Jimbo la KKKT Katavi, mchungaji Daud Moshi,
mchungaji kiongozi wa usharika Zebedayo Mbilinyi na wajumbe wa kamati ya
uongozi ya dayosisi hiyo.
Askofu huyo
pamoja na kufika kwa ajili ya kushiriki ibada ya jana, pia ilikuwa amtambulishe
rasmi Mchungaji Mbilinyi katika kituo chake kipya cha kazi kumrithi Calvin
Kessy aliyepewa barua ya uhamisho.
Kwa muda wa
siku tatu mfululizo mpaka jana askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha
Jeshi la Polisi walikuwa wakishinda katika eneo la kanisa hilo, ili kulinda
usalama kutokana na hofu ya kuibuka ghasia.
Baada ya Askofu
Mbilinyi kufika kanisani hapo jana akiwa ameongozana na ujumbe huo na akidhani
angekwenda moja kwa moja ndani ya kanisa, waumini walianza kuimba nyimbo za
kumkataa na baada ya muda walianza kumrushia mawe.
Kitendo cha
kupigwa mawe kilisababisha askofu huyo na ujumbe wake kila mmoja kukimbilia
ndani ya gari lake na kuondoka, wakiwaacha FFU wakijaribu kutuliza waumini hao.
Baada ya FFU
kufanikiwa kutuliza vurugu hizo, baadhi ya waumini waliingia kanisani na
Mwinjilisti Aniseth Msangawale aliyeongoza ibada mpaka mwisho kabla ya
kutawanyika kurejea makwao.
Baadhi ya
waumini hawataki kumuona askofu huyo akisali katika usharika mkuu huo kwa madai
ya kumhamisha kinyume cha utaratibu mchungaji wao.
UBABE NA
HILAWaumini hao wamekuwa wakipinga kuhamishwa kwa Mchungaji Kessy wakidai
uhamisho wake umefanyika kwa ubabe na hila, na kwamba amenyimwa hata fursa ya
kuwaaga licha ya kuwaongoza kwa muda mrefu.
Aidha, waumini
hao wanadai kuwa uhamisho wa mchungaji Kessy umetokana na maslahi binafsi
ambapo baadhi ya wajumbe wa kamati ya dayosisi hawataki kumuona mchungaji huyo
kwa kuwa amekuwa akifuatilia na kudhibiti mapato ya Usharika wa Sumbawanga
Mjini walio ndani na nje kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Dayosisi ya
Tanganyika.
Akizungumza na
gazeti hili, Katibu wa Dayosisi ya Tanganyika, Fredrick Nyamoga alisema waumini
wanaogomea uhamisho wa Mchungaji Kessy wanapaswa kutii mamlaka kwani ni wa
kawaida.
Naye mmoja wa
waumini hao, Baraka Lyimo alisema hawakatai kuhamishwa kwa Mchungaji Kessy,
lakini wasichofurahia ni mchungaji huyo kupewa uhamisho baada ya mvutano
kuibuka baina yake na Askofu Mwaipopo.
Zelubaberi
Luvanda, muumini wa usharika huo alisema Mchungaji Kessy alikuwa akijitahidi
kuhamasisha waumini kuchangia michango kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo
sambamba na kudhibiti matumizi hali iliyosababisha apewe uhamisho.
Chanzo- Nipashe




