Msanii Ali Kiba (King Kiba) Aburuzwa Mahakamani

Mfanyabiashara
wa mitumba Hadija Hassan amefungua kesi ya madai ya matunzo ya mtoto dhidi ya
msanii nguli wa muziki wa kizazi kipya, Ali Kiba maarufu kama King Kiba.
Katika kesi hiyo,
Hadija anadai jumla ya Sh. milioni 1.41, ikiwamo Sh. 950,000 za ada na Sh. 460,000
za matumizi ya mtoto wa miaka mitano (jina limehifadhiwa kwa sababu za kisheria
na kimaadili).
Hadija ambaye ni
mfanyabiashara wa mitumba amefungua kesi ya madai hayo katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam akidai matunzo kwa mlalamikiwa ambaye
ni mzazi mwenzie -King Kiba.
Kwa mujibu wa hati
ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo, mlalamikaji anadai kuwa Januari, 2013
katika Hospitali ya Mikocheni, jijini Dar es Salaam alizaa mtoto wa kike ambaye
baba yake ni mlalamikiwa.
Alidai kupitia
hati hiyo kwamba mlalamikiwa anatakiwa kumhudumia mtoto huyo kwa mahitaji yote
muhimu ikiwamo chakula, nguo, elimu na matibabu.
"Kutokana na
Sheria ya Watoto ya mwaka 2009, mdaiwa anatakiwa kutoa huduma kila mwezi,
chakula Sh. 150,000, matunda Sh. 50,000, chakula cha ziada Sh. 50,000, michezo
na burudani za watoto Sh. 100,000, nguo Sh. 60,000 na matibabu Sh. 50,000
ambapo jumla ni Sh. 460,000," alidai mlalamikaji kupitia hati hiyo.
Aidha mlalamikiwa
anatakiwa kulipa ada ya shule kwa muhula Sh. 950,000, na anadaiwa aliacha kutoa
matunzo hayo kwa mtoto tangu Januari, mwaka huu hivyo anaiomba mahakama
imwamuru mdaiwa kutoa matunzo hayo ya Sh. 460,000 kila mwezi na ada.
Pamoja na mambo
mengine, mlalamikaji anaomba malipo ya kwanza yatolewe mapema baada ya hukumu,
na pia anaiomba mahakama imwamuru King Kiba kumsomesha mtoto, kumnunulia nguo
na matibabu ikiwamo kumtafutia bima ya afya.
Pia mlalamikaji
anaomba mahakama imwamuru Kiba kulipa gharama za matunzo Sh. 460,000 kuanzia
Februari 2017 mpaka siku itakapotolewa hukumu na gharama za kesi ziwe kwa
mdaiwa.
Mbali na maombi
hayo, Hadija anaomba mahakama itoe amri nyingine yoyote itakayoona inafaa kwa
manufaa yake. Kesi imefunguliwa kwa msaada wa Kituo cha Wanawake cha Msaada wa
Kisheria (WLAC).
Ali Kiba, ambaye
jina lake la kuzaliwa ni Ali Saleh Kiba amefunguliwa madai hayo ikiwa ni siku
chache tangu afunge ndoa iliyopendeza mjini Mombasa Kenya.



