Breaking News

Ubalozi Wa Kuwait Watoa Vifaa Kwa Watu Wenye Ulemavu.

Na Maneno Selanyika
TAASISI isiyo ya Kiserikali ya Humanity Action For Children Faundation kwa kushirikia na Ubalozi wa Kuwait nchini imetoa msaada wa vifaa kwa watu wenye ulemavu vyenye thamani ya zaidi ya Mil 11.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kukabidhi msaada huo, Mwanzilishi wa Taasisi hiyo, Bi. Rahma Mohamed, alisema vifaa vilivyotolewa ni Baiskel za walemavu, Fimbo maalum za kutembelea pamoja na magongo.

Alisema wanufaika na msaada huo ni Walemavu wa kuona, walemavu wa viungo pamoja na watu wenye Ualbino ambao ni zaidi ya 110.

“Ubalozi wa Kuwait umejiwekea utaratibu wa kutenga fungu la fedha ambazo huzigawa kwa taasisi ambazo zinahusika na masuala ya kusaidia watu wenye mahitaji maalum… vifaa hivi ni kutokana na mpango huo” alisema Bi. Rahma.
Aidha Bi. Rahma aliongeza kuwa Lengo ni kuwasaidia watu wenye uhitaji wa vifaa mbalimbali lakini hawana uwezo wa kumudu kuvinunua kwahiyo ni tumie fursa hii kuwaomba wavitumie kulingana na dhumuni na msukumo wa ubalozi katika msaada huu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Seif Jega, alisema walemavu wa kuona wamekuwa na changamoto ya fimbo maalum kwani zinauzwa kwa bei kubwa ambapo wengi hawawezi kuzinunua.

“Fimbo hizi ndizo nyenzo muhimu ya kutusaidia kutembea lakini zinauzwa kwa gharama kubwa kati ya Sh 50,000 na 60,000 wengi wetu hatuwezi kununua hivyo inakuwa changamoto katika harakati zetu,” alisema Bw. Jega. 
Alisema vifaa walivyokabidhiwa vitakuwa na msaada mkubwa kwao kwa sababu vitawasaidia kutoka sehemu moja kwenda pengine kwa ajili ya kujitafutia kipato.