Mawaziri Wanne, Spika Ndugai Watifuana Vikali Bungeni

Waziri wa Katiba
na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi (kushoto) na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista
Mhagama (kulia), wakijadili jambo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk.
Adelardus Kilagi, bungeni Dodoma jana. | Picha na John Dande
***
BAJETI ya Wizara
ya Maliasili na Utalii, imepitishwa huku kukitokea msuguano mkali kati ya Spika
wa Bunge, Job Ndugai, wabunge na mawaziri wanne waliokuwa wanajibu hoja
zilizotolewa.
Dalili za ugumu wa
upitaji wa bajeti hiyo zilianza kuonekana wakati wa kikao cha asubuhi wabunge
walipokuwa wakali juu ya utekelezaji mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge
na athari za mazingira zinazoweza kutokea katika Pori la Akiba la Selous, huku
Spika Ndugai alionekana kuungana nao.
Pia kiongozi huyo
wa Bunge, alionekana kuungana na wabunge juu ya udhaifu ulio kwenye kuweka
mipaka katika mbuga za wanyama na mapori tengefu.
Hoja nyingine
ambazo wabunge waliziibua, ni ukuzaji wa utalii nchini na wananchi
kunyang’anywa mifugo na watu wa hifadhi.
Hali hiyo ilikuja
kujidhihirisha jioni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kujadili bajeti ya
wizara hiyo inayosimamia sekta ya utalii, ikikadiriwa kuchangia asilimia 17.2
ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni.
Katika hali hiyo,
mawaziri wanne ilibidi wasimame kuinusuru, ambao ni Dk. Hamisi Kigwangalla
(Maliasili na Utalii), Dk. Merdad Kalemani (Nishati), Mhandisi Isack Kamwelwa
(Maji na Umwagiliaji) na Kangi Lugola (Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira).
MTIFUANO
ULIVYOANZA
Hali hiyo ilitokea
baada ya Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM), kutishia kushika shilingi ya
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Kigwangalla kama Serikali itashindwa kumpa
majibu ya madhara ya watu watakaopitiwa na mradi wa huo.
“Mheshimiwa Spika,
nilikuwa naomba ‘commiment’ ya Serikali kwani mradi utakaotekelezwa utakuwa
katika zaidi ya hekta 85,000.
“Kwahiyo, nilikuwa
naomba Serikali ‘iji-commit’ kwa wale watakaopisha mradi wawe kipaumbele katika
mradi huo ambao utatokana na Bonde la Mto Rufiji,” alisema Mlinga.
Akilitolea
ufafanuzi suala hilo, Dk. Kigwangalla alisema. “Kwanza ni ngumu sana kuja
kubaini kwamba hawa ndio wanakuja kunufaika na programu ya umwagiliaji katika
hatua hii ya sasa.
“Lakini pia ni
ngumu kwani kuna wananchi ambao watatolewa kupisha mradi wa Stiegler’s Gorge
kwa sababu hilo halipo, kwani mradi utatekelezwa katika pori la akiba na
hautekelezwi Wilaya za Malinyi, Kilombero.
“Lakini pia,
tunachora mipaka upya kwa Kilombero Game Control Area, tumeachia eneo kubwa
sana kwenye vijiji, kwa sababu mwanzoni ilikuwa na ukubwa kilomita 7,500 na leo
hii tumepunguza mpaka 2,500.
“Tunatengeneza
miradi ya skimu za umwagiliaji ili kutumia maji hayo ili Mto Kirombero
usiharibike.”
Pamoja na majibu
hayo, Mlinga hakuridhika na kuomba kwa Spika Ndugai kutoa hoja ili wabunge
waijadili.
“Mheshimiwa Spika,
hivi ninavyoongea, jimboni hakukaliki na sio Ulanga tu, Malinyi, Kilombero na
Mlimba pia. Sasa naona mheshimiwa waziri anachukulia kama masihara, nomba
wabunge wenzangu mniunge mkono tujadili suala hili,” alisema Mlinga na kuungwa
mkono na wabunge wenzake.
Pamoja na kutoa
hoja hiyo, Spika Ndugai alidai mbunge huyo hakusema kitu chochote kuhusu nia
yake hiyo.
Baada ya kuona
suala hilo linawagusa wabunge wengi, Spika Ndugai alitaka Wizara ya Nishati
nayo ilizungumzie.
“Mheshimiwa Waziri
wa Nishati, kwenye hii hoja ambayo inasemwa miti sijui milioni ngapi itakatwa,
Stiegler’s Gorge na athari ambazo zitatokea, Tanesco hawajihusishi na miradi ya
mazingira, lazima waanze kujihusisha na utunzaji wa mazingira.
“Yaani, badala ya
Tanesco kujishughulisha na umeme pekee, lazima wajue wanawajibika kwa kiasi
fulani katika mazingira,” alisema Spika.
Hoja hiyo
ilimwibua Dk. Kalemani aliyesema kuna mambo mawili ya kufanya katika mradi huo.
“Ni sahihi
mheshimiwa mbunge, lile bwawa ambalo litajengwa litaweza kuhifadhi maji za
hekta za umwagiliaji zaidi ya 250,000 na maji hayo yatasaidia.
“Mradi haujaanza
kutekelezwa, taratibu zitazingatiwa, sio kwamba mradi utaanza tu, na hadi saa
hakuna mti hata mmoja uliokatwa,” alisema Dk. Kalemani.
Baada ya hatua
hiyo, Spika alimruhusu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Kamwelwe ambaye alisema
skimu ya umwagiliaji itakapokamilika, watu watakaopewa nafasi ya kwanza ni wale
wanaoishi katika maeneo hayo.
Kwa upande wake,
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisimama na kuomba
taarifa akidai miradi ya umwagiliaji haiisaidii nchi.
“Mwenyekiti,
nilikuwa nataka tunapojadili mambo ya kitaifa, tuwe wakweli kwa saababu tuna
mifano ambayo tayari tumeishaiona kwa Mkoa wa Dodoma ambapo Mtera wana bwawa,
lakini hakuna umwagiliaji, Kidatu wana bwawa, lakini hakuna umwagiliaji na
Kihansi wana bwawa, lakini hakuna umwagiliaji.
“Mimi nadhani hoja
ya msingi ni hii ambayo Mwenyekiti umeileta, kwamba kuna ukataji wa miti
shirika ambalo linanufaika na mradi lazima lije na hoja.
“Hayo ndiyo
maelekezo yachukuliwe na Serikali, siyo blabla zinazoletwa hapa,” alisema
Zitto.
Akilitolea
ufafanuzi hilo, Dk. Kalemani alisema kila mradi una ‘dizaini’ yake na mradi wa
Stiegler’s Gorge ni wa kisasa.
“Ethiopia ambayo
ina jumla ya megawati 4,822 inatekeleza mradi mwingine mkubwa zaidi ya megawati
6,450 lakini kwa ‘dizaini’ ya mradi huu ni tofauti kabisa.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mtera kuna hifadhi kama ya Selous kwa vyovyote lazima ‘dizaini’
zitofautiane, hivyo baianuai haiwezi kuathirika,” alisema.
Kutokana na
maelezo hayo ya Dk. Kalemani, Spika Ndugai alisema waziri huyo hajawaelewa hata
kidogo.
“Mheshimiwa Waziri
yaani hujatuelewa kabisa, yaani suala letu ni dogo sana. Katika mambo ya
mazingira kuna hiyo miti ambayo itakatwa, hilo ni lazima lifanyike wala
hatulaumu.
“Bwana Tanesco
anatakiwa kuwa pia na mawazo ya mazingira baadae huko,” alisema Spika huku
akishangiliwa na wabunge.
Kutokana na
maelezo hayo, Dk. Kalemani aliomba nafasi ya kutaka kulifafanua hilo lakini
Spika alimkatalia.
Akilitolea
ufafanuzi hilo, Kigwangalla alisema: “Tunakubaliana na mapendekezo yako na
ndiyo mapendekezo ya wizara yetu, sisi tumepeleka mapendekezo katika kamati
ambapo tunataka tutumie kanuni ya PPP ili itengenezwe tozo kwa ajili ya jambo
hilo.
“La pili, katika
uvunaji wa miti kuna matarajio ya kuuza miti hiyo kibiashara, tunaivuna, katika
uvunaji kuna mauzo yatafanyika na mauzo yake yana thamani ya kati ya Sh bilioni
400 mpaka 600, hizi pesa zitatumika katika uhifadhi wa maeneo hayo.
“Hili suala la
vigingi, kuna maeneo nimekwenda nikakuta kuna misikiti, nyumba za watu na
makanisa vimewekwa vigingi.
“Kwahiyo, niko
tayari kumwomba Mheshimiwa Rais akubali kubadilisha sheria ili maeneo hayo
yanayoonekana kuwa katika maeneo ya hifadhi, yaruhusiwe kuendelea kuwapo,”
alisema Kigwangalla.
Kuhusu mapori ya
akiba, alisema baadhi yake yatapandishwa hadhi na barabara zinazoelekea katika
maeneo hayo, zitajengwa ili kurahisisha usafiri.
Naye Lugola,
alisema lazima mradi huo utatekelezwa na atakayeupinga, atafungwa.
Pamoja na hayo,
aliwataka wabunge warejee ripoti ya Profesa Raphael Mwaryosi aliyoitoa na kueleza
jinsi mradi huo utakavyotekelezwa.
CHANZO - MTANZANIA



