Mkuu Wa Wilaya Amuweka Mahabusu Mwenyekiti Wa Ccm

Mgogoro
unafukuta wilayani Mwanga ambako mkuu wa wilaya hiyo, Aaron Mbogho anadaiwa
kumuweka mahabusu mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Jaffary Kandege.
Kwa
kawaida kiongozi wa CCM kwa ngazi kama hiyo, anatakiwa kuwa juu ya kiongozi wa
Serikali kutokana na chama hicho kuwa kimeshika Serikali.
Lakini
mkuu huyo wa wilaya aliagiza apelekwe kituo cha polisi.
Taarifa
zinadai kuwa mwenyekiti huyo wa CCM aliwekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi
Mwanga Ijumaa wiki iliyopita kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 8:00 usiku kabla
ya kudhaminiwa na diwani wa Shighatini (CCM), Enea Mrutu.
Akizungumza
na Mwananchi, mwenyekiti huyo alisema kwa hali ya mgogoro huo ilipofikia,
hayupo tayari kufanya kazi na DC huyo kwa kuwa amekidhalilisha chama na yeye
binafsi.
Tukio la
kukamatwa kwa Kandege limekuja wiki moja tangu kikao cha baraza la madiwani wa
wilaya kidai kuwa hawana imani na mku huyo wa wilaya na kamati yake ya ulinzi
na usalama.
Kauli ya
madiwani hao ilitokana na kuendelea kukithiri kwa uvuvi haramu katika Bwawa la
Nyumba ya Mungu, huku baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi na maofisa maliasili
wakinyooshewa kidole kwa kukosa uadilifu.
DC atema
cheche
Hata
hivyo, DC Mbogho amedai Kandege hakufikishwa polisi na kuhojiwa kwa wadhifa
wake wa mwenyekiti wa CCM wa wilaya.
“Muulizeni
aliandikisha maelezo kuhusu tuhuma gani? Ukipelekwa mahabusu kwa amri ya DC
huwa huandiki maelezo ya kijinai. Hajahojiwa kama mwenyekiti wa CCM, bali
Jaffary Kandege,” alidai Mbogho.
Kwa
mujibu wa mkuu huyo wa wilaya kama kosa analotuhumiwa nalo, lingekuwa linahusu
wadhifa wake wa uenyekiti wa CCM wilaya, lingeshughulikiwa kwa mujibu taratibu
za kichama.
Mbogho
alidai kuwa wao kama kamati ya ulinzi na usalama walipokea taarifa kuwa Kandege
anahusishwa na tuhuma za kushawishi wananchi kuwashambulia maofisa na magari ya
Serikali.
“Alipelekwa
pale kwa tuhuma za uchochezi na alipokuja ofisini kwangu nilimwambia waziwazi
kuwa unatajwa katika hili na itabidi ukaandike maelezo polisi. Wala hakuwekwa
kwa saa 48,” alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.
“Huyo mtu
ana matatizo yake binafsi asiyafiche kwenye chama changu. Umma utenganishe mtu
na wadhifa. Mhalifu atabaki kuwa mhalifu tu na sheria itachukua mkondo wake
bila uonevu.”
Mkuu huyo
wa wilaya alisema ni utaratibu ulio wazi kuwa mshukiwa wa uhalifu ni lazima
ahojiwe na kudhaminiwa, na kwamba Kandege huenda alikaa polisi kwa muda huo
akisubiri kudhaminiwa.
Alidai
kumekuwapo na matukio ya maofisa wa maliasili na polisi wanaokwenda kudhibiti
vitendo vya uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu kushambuliwa kwa mawe
na baadhi ya wananchi.
Malalamiko
ya Kandege
Hata
hivyo, Kandege aliiambia Mwananchi kuwa kitendo cha kuwekwa mahabusu kinatokana
na chama kumtaka DC Mbogho awape taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM.
“Nilipowekwa
mahabusu tumetafakari sana na wenzangu ndani ya CCM na kujiuliza kulikoni?
Tatizo nini? Tukajiuliza labda ni kwa sababu tumemtaka atuletee taarifa ya
utekelezaji wa ilani,” alisema.
“Ameona
afanye hivyo ili kunipunguza nguvu, lakini nitaendelea kupaza sauti pale ambapo
naona mambo hayaendi sawa. Kila tukimtaka kwenye kamati ya siasa alete taarifa,
haleti.
“Tabia ya
kuwawekaweka watu ndani ikome kwa sababu si nzuri. Ameshawaweka mahabusu
watendaji wengine wa Serikali. U-DC isiwe ndio fimbo ya kuwatandika watendaji
wa Serikali.”
Mwenyekiti
huyo alisema mwezi Januari, mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alifanya
mkutano katika kitongoji cha National uliohudhuriwa pia na mkuu huyo wa wilaya.
“Kwenye
ule mkutano wananchi walilalamika kuwa baadhi ya polisi na maofisa maliasili
wanapokamata makokoro, wanachukua fedha nyingi na kuachia makokoro,” alisema
Kandege.
“Kwanza
nilikemea vikali tabia ya wananchi kupiga mawe watendaji wa Serikali
wanapotekeleza majukumu yao, lakini nikawataka polisi na maofisa maliasili
wanaolalamikiwa nao wawe waadilifu.
“Vyombo
vyote vya ulinzi na usalama mkoa na wilaya vilikuwapo na nilisema kwa ujumla
wake. Nashangaa leo kuitwa na kuhojiwa na kubambikiwa kesi ya uongo ya
kushambulia gari la polisi.”
Mwenyekiti
huyo alidai mkuu huyo wa wilaya ana mgogoro na kamati ya siasa ya wilaya, kwa
vile kila anapopelekewa barua ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani,
hafanyi hivyo.
RPC,
katibu wa CCM wanena
Kamanda
wa polisi wa mkoa, Hamis Issah hakutaka kuzungumzia suala hilo na kuelekeza
atafutwe mkuu wa Wilaya ya Mwanga kwa kuwa ana mamlaka ya kulizungumzia.
Lakini
katibu wa CCM wa wilaya, Mwanaidi Mbisha alisema wanashughulikia suala hilo
ndani ya chama.
“Jambo
hili ni la kichama. Tunalishughulikia wenyewe (CCM) kwa hiyo mliache kama
lilivyo,” alieleza Mbisha.
Viongozi,
wana CCM wafunguka.
Viongozi
wa kisiasa na baadhi ya wanachama wa CCM waliohojiwa na Mwananchi, walidai
kushtushwa na kitendo cha DC huyo na kutaka chama kiingilie kati.
“Kiukweli
mimi naona kuna visa fulani na moja ni hili la madiwani kumkataa DC. Labda
anaona chama kina mkono wake. Yule (Kandege) ni kiongozi, haikuwa busara
kumuweka mahabusu,” alisema diwani wa Shighatini (CCM), Mrutu aliyemdhamini
mwenyekiti wake.
Mrutu
alisema anachofahamu ni kuwa katibu wa CCM wa wilaya hiyo ameshaagizwa kuitisha
kikao cha halmashauri ya wilaya ili kujadili suala hilo ambalo alidai
limewaudhi wanachama, na kisha kutoa msimamo wa chama.
Kwa
upande wake, mwenyekiti wa Kijiji cha Ruru (CCM), Juma Rehani alisema kuwa
hawaridhishwi na utendaji wa mkuu huyo wa wilaya na ndio maana walitishia
kuhamia nchi jirani ya Kenya.
Das
alivyoswekwa mahabusu
Hii si
mara ya kwanza kwa DC Mbogho kutuhumiwa kuamuru viongozi kusekwa ndani.
Inadaiwa
kuwa Agosti 10, 2017, mkuu huyo wa wilaya aliamuru kuwekwa mahabusu kwa katibu
tawala wake (Das), Yusuph Kasuka, lakini DC akasema hakuwekwa ndani kwa sababu
ya wadhifa wake, bali kama Kasuka.
Kasuka
alikaririwa na Mwananchi akisema hafahamu sababu wala kiini cha kukamatwa bali
polisi walifika ofisini kwake kumchukua na kutaka sababu za kukamatwa kwake
aulizwe mkuu wa wilaya.
Lakini
taarifa zilidai baadaye kuwa DC aliamua kuchukua uamuzi wa kulipeleka suala la
Das wake polisi baada ya kunusa harufu ya ufisadi katika matengenezo ya gari
mojawapo la ofisi yake.
CHANZO-MWANANCHI



