Mtoto Wa Baba Wa Taifa 'Nyerere' Amshangaa Rais Magufuli
MTOTO wa Hayati
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, amesema ameshangazwa
na uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli kumteua kuwa Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi CCM) kwa kuwa hakuwahi kuwaza kupata
nafasi hiyo.
Makongoro ambaye
ni mtoto wa nne kuzaliwa kwa Baba wa Taifa anakuwa wa kwanza katika familia
hiyo kuwa mjumbe wa NEC.
Mwenyeti wa CCM,
Rais Magufuli, jana alitangaza kuwateua Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na
Makongoro Nyerere kuwa wajumbe NEC.
Akizungumza na
Nipashe jana kwa njia ya simu, Makongoro alisema: “Rais Magufuli ambaye pia ni
mwenyekiti wangu wa chama amenishangaza kati ya nafasi zake zisizozidi saba za
kuteua wajumbe wa NEC ameniteua na mimi.”
“Amenipa heshima
kubwa sana kuniteua katika nafasi zake za kwanza tena na Waziri Mkuu Mstaafu
Mizengo Pinda ambaye ni kiongozi ninayemheshimu sana,” alisema Makongoro.
Alisema Rais
Magufuli mara kwa mara amekuwa akitoa ahadi kwa Watanzania kuwa hatawaangusha
katika utendaji kazi wake na hivyo kumteua kwake ni heshima kubwa.
Kuhusu uteuzi huo,
Makongoro alisema hakuwa anafahamu jambo lolote na wala hakutarajia kupatiwa
nafasi hiyo ya juu.
Alisema amekuwa
akijishughulisha na kazi zake binafsi katika kipindi cha mwaka mmoja tangu
akose nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki, mwaka jana.
Makongoro pia
alisema neema ya uteuzi huo imekuja wakati ambao ni msimu wa mwezi Mtukufu wa
Ramadhani unaowalazimu Waislam kote nchini kufunga ili kutimiza nguzo za dini
hiyo.
Kadhalika,
Makongoro aliahidi kuwa mtumishi na mwanachama mwaminifu wa CCM na uadilifu
mkubwa.
“Katika utumishi
wangu kwa nafasi niliyoteuliwa ya mjumbe wa NEC nitakuwa mwadilifu kwa
kuwasilisha matatizo ya wanachama na kuhakikisha yanasikilizwa na kufanyiwa
kazi,” alisema Makongoro.
Aprili 24, mwaka
huu, wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa benki ya NMB mkoani Dodoma, Makongoro
alimwomba Rais Magufuli ampe kazi kwa sababu yeye ni mchezaji wa akiba
akisubiri kuanza kazi.
Aliposimama
kuzungumza kwenye tukio hilo, Rais Magufuli alisema Makongoro anastahili kuwa
mchezaji wa nafasi ya kwanza na si mchezaji wa akiba.
Makongoro Nyerere ni nani?
Alizaliwa Januari
30, mwaka 1959 na katika maisha yake siasa aliwahi kujiunga na chama cha
upinzani cha NCCR-Mageuzi mwaka 1995.
Mwaka huo huo
alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kwa tiketi ya chama hicho,
lakini alidumu kwa miaka miwili katika nafasi hiyo.
Mwaka 1997
Mahakama Kuu ya Tanzania ilitengua ubunge wake na uchaguzi uliofuata Felix
Mrema wa CCM alichukua nafasi hiyo.
Mwaka 2000 ikiwa
ni mwaka mmoja baada ya baba yake Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere
kufariki, alijiunga na CCM.
Mwaka 2004 Rais wa
awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alimteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Mwaka 2007 akiwa
kada wa CCM, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mara nafasi
aliyodumu nayo hadi mwaka 2012.
Mwaka 2012 Makongoro,
alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kati ya
wabunge nane kutoka Tanzania.
Mwaka 2015
Makongoro alikuwa miongoni mwa vigogo 38 wa CCM waliochukua fomu ya kutaka
kuteuliwa na chama hicho kuwania nafasi ya urais ingawa hakufika mbali.
Chanzo- Nipashe



