Rais MAGUFULI Aikabidhi Simba Kombe Baada Ya Kipigo Cha Goli 1-0 Kutoka Kwa Kagera Sugar

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk, John Pombe Joseph Magufuli amewakabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Simba SC wakitoka kufungwa 1-0 na Kagera
Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mei 19, 2018.
Kabla ya kuwakabidhi Kombe hilo, Rais
Magufuli akawaambia Simba SC hajaridhishwa na kiwango cha mchezo wao na
akawataka wakakiboreshe kuelekea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika
mwakani.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli
amewapongeza Simb SC kwa kufikia kutwaa la ubingwa wa Ligi Kuu bila ya kupoteza
mechi kabla ya kufungwa na Kagera leo.
“Mimi huwa ninafuatilia ligi
mbalimbali, nilifuatilia hadi juzi timu ambazo zilikuwa zimechukua ubingwa bila
kufungwa, zilikuwa zimebaki mbili, Barcelona na Simba, Jumapili iliyopita
Barcelona wakafungwa na leo Simba nao wamefungwa,”alisema Rais Dk. Magufuli
kabla ya kuwakabidhi Kombe hilo Simba SC.
Rais amesema kwamba anawapongeza
Simba SC kwa sababu pia wamepitia kipindi kirefu bila kuchukua ubingwa na
akasema anazipongeza na timu nyingine zilizoshiriki Ligi Kuu msimu huu huku
akiwatania SImba; “Nashukuru hakuna timu iliyokwenda FIFA (Shirikisho la Soka
la Kimataifa) kudai pointi za mezani msimu huu,”.
Aidha, Rais Magufuli aliyewapongeza
Kagera Sugar kwa kuonyesha mchezo mzuri leo pia alisema Simba SC nayo
ilijitahidi na kudhihirisha wao ni mabingwa.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na
marefa Florentina Zablon wa Dodoma aliyesaidiwa na Jesse Erasmo wa Morogoro na
Mashaka Mwandile wa Mbeya, bao pekee la Kagera Sugar limefungwa na mshambuliaji
wa zamani wa Simba SC, Edward Christopher Shijja kwa kichwa dakika ya 84
akimalizia krosi ya Japhet Makalai kutoka upande wa kulia.
Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi
akapoteza nafasi ya kuisawazishia Simba SC dakika ya nne ya muda wa nyongeza
baada ya kukamilika kwa dakika 90 za kawaida kufuatia mkwaju wake wa penalti
kupanguliwa na kipa Juma Kaseja.
Florentina Zablon aliwapa Simba
penalti hiyo baada ya Okwi mwenyewe kuangushwa na kiungo mkongwe wa Kagera
Sugar, George Kavilla.
Simba SC inabaki na pointi zake 68
baada ya kucheza mechi 29 na itakwenda mjini Songea kukamilisha msimu kwa
kumenyana na wenyeji Maji Maji Mei 28 Uwanja wa Maji Maji. Kagera Sugar
inafikisha pointi 34 katika mechi ya 29, ingawa wanabaki nafasi ya 10.
Kikosi cha SimbaSC kilikuwa; Said
Mohamed Nduda, Nicholas Gyan/Muzamil Yassin dk46, Mohammed Hussein
‘Tshabalala’, Paul Bukaba, James Kotei/Salim Mbonde dk50/John Bocco dk70,
Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco, Shiza
Kichuya,
Kagera; Juma Kaseja, Suleiman
Mangoma, Abdallah Mguhi, Juma Nyoso, Mohamed Fakhi, Peter Mwalyanzi, Japhet
Makalai, Ally Ramadhani/George Kavilla dk58, Japhery Kibaya/Paul Ngalyoma dk79,
Edward Christopher, Atupele Jackson/Omar Daga dk32.



