Rais MAGUFULI Amnyima Kijana Nauli, Amtaka Akalime

Rais John Magufuli amemnyima fedha
kijana mmoja aliyemuomba kiongozi mkuu huyo wa nchi nauli, wakati alipokwenda
kwa mamantilie eneo la Bandari Dar es Salaam kunywa chai muda mfupi,
baada ya kumaliza ziara yake ya kushtukiza katika bandari hiyo.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Mei
15, 2018 wakati akinunua mapapai na ndizi baada ya kukuta chai ikiwa imekwisha
katika genge la mamantilie huyo, huku kijana aliyekuwa akimsaidia mama huyo
kupiga hesabu za matunda hayo, kuchomekea suala la nauli.
“Nataka mapapai nikale na wenzangu pale.
Wewe mama jumlisha bei ninunue tena wewe mhehe si ndio, unaona sasa mtani wangu
wewe. Haya haya hapa shilingi ngapi?,” amesema Magufuli akiuliza bei ya mapapai
na kujibiwa kuwa ni Sh22,000.
“Na hizi ndizi ni kiasi gani, sawa kwa
hiyo hizi ndizi zote pamoja na mapapai ni Sh23,000 si ndio. Sasa mimi
nakuongeza nakupa Sh30,000 kabisa, au hutaki hela yangu mama.”
Baada ya mama huyo kupokea kiasi hicho
cha fedha, kijana huyo alimuomba Rais nauli, “mheshimwia rais naomba nauli.”
“Hakuna nauli hapa nenda kalime,”
amesema Rais Magufuli na kuwafanya waliokuwepo eneo hilo kuangua kicheko.



