Serikali Yasema Haina Mpango Wa Kurekebisha Sheria Ya Mtandao

Serikali imesema tangu kuanza kwa
matumizi ya sheria ya makosa ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015, imesaidia
kupunguza makosa ya mtandao na upatikanaji wa haki pale mtu anapotenda kosa
tofauti na awali hivyo hawana mpango wowote kwa sasa kufanya marekebisho kwenye
sheria hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mei 21,
2018 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa
Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 33 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la nyongeza la Mbunge wa Ubungo
Said Kubenea aliyetaka kujua lini serikali itapeleka bungeni mswada wa
marekebisho ya sheria mtandao inayobana uhuru wa mwananchi kupata habari.
"Uwepo
wa sheria ya makosa ya mtandao Na. 14 ya mwaka 2015 umesaidia kupungua kwa
makosa ya kimtandao, upatikanaji wa haki pale mtu anapotenda kosa kwani kabla
ya hapo kulikuwepo na changamoto na uanishaji wa makosa na adhabu hali
iliyopelekea haki kutopatikana", amesema Kwandikwa.
Pamoja na hayo, Kwandikwa ameendelea
kwa kusema "uwepo wa sheria
hiyo umewezesha kuimarika kwa matumizi salama ya mtandao na kuleta maendeleo
kwa wananchi. Sheria hii ni muhimu sana kwa nchi yetu na badala ya kuwaathiri
watumiaji au wananchi imesaidia kupunguza waharifu wa mtandao.....
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Jeshi la Polisi inaonyesha kupungua kwa makosa hayo kwa asilimia 48.9 kati ya
Januari hadi Disemba 2017. Hivyo kwa sasa serikali haina mpango wa kupeleka
marekebisho ya sheria hiyo bungeni hadi hapo kutakapokuwa na uhitaji wa kufanya
hivyo".
Kwa upande mwingine, Kwandikwa
amewataka wananchi kutumia fursa chanya zitokanazo na matumizi sahihi ya
mitandao kuliko kutumia mitandao hiyo kuvunja sheria za nchi na maadili pamoja
na tamaduni za kitanzania.



