TRA Yakomaa Na Makontena Ya RC Makonda, Yaeleza Sababu Za Kutomsamehe Kulipa Kodi
Picha Na Mtandao
Dar es salaam:
Kitendo cha nyaraka za makontena 20
yenye samani yaliyo katika hatari ya kupigwa mnada na Mamlaka ya Mapato (TRA)
mwezi ujao kuwa na jina la mtu binafsi Paul Makonda,ni moja ya sababu
zilizomkwamisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kusamehewa ushuru wa forodha na
kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kama alivyoomba, imefahamika.
Kwa mujibu wa barua ya Waziri wa Fedha
na Mipango, Philip Mpango kwa 'RC' Makonda ya Machi 24, mwaka huu kwa mujibu wa
sheria, shehena hiyo ya samani haistahili kupata msamaha wa ushuru wa forodha
au bidhaa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa sababu kadhaa ikiwamo
kuonekana kuwa mali ya mtu binafsi.
Makonda aliiandikia wizara barua Januari
3, mwaka huu akiomba msamaha wa kodi kwenye samani za shule za Mkoa wa Dar es
Salaam zenye thamani ya "takribani" Sh. bilioni 1.4 ambazo alidai ni
msaada kutoka kwa wananchi wapenda maendeleo waishio Marekani.
Ombi hilo hata hivyo limekataliwa na
Waziri Mpango kwa kuzingatia Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
ya mwaka 2004 na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014.
Barua ya Dk. Mpango inasema kwa mujibu
wa Sheria ya VAT, msamaha kwa taasisi za Serikali ni kwa shughuli zisizo za
kibiashara, "kwa masharti kwamba usiwepo uwezekano wa shughuli kama hiyo
kutolewa na taasisi isiyo ya kiserikali".
Kwa mujibu wa barua hiyo ya Wizara ya
Fedha, samani kama hizo zinaweza kutolewa na taasisi isiyo ya kiserikali au mtu
binafsi hivyo kuwa nje ya eneo la msamaha.
Aidha, Makonda amekataliwa msamaha wa
kodi kwa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa siyo asasi ya kiraia au taasisi ya kidini, barua
hiyo inasema na kufafanua:
"Magazeti ya Serikali namba 205 na
206 ya mwaka 2016 yanatoa misamaha ya ushuru wa forodha na wa bidhaa kwa asasi
za kiraia na taasisi za dini kwa vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya kuendeleza,
kuanzisha au kukarabati miradi inayolenga elimu, usambazaji maji, huduma za
afya na miundombinu."
Viti, meza na mbao za darasani
vinavyodaiwa kuwamo katika mzigo wa Makonda vinaonekana kuangukia nje ya
jedwali hilo.
Mbali na majibu kwa Makonda, nakala ya
barua ya Waziri Dk. Mpango imepelekwa pia Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu, Tamisemi,
Wizara ya Fedha na TRA.
Alipoulizwa jana kwa njia ya simu kama
Makonda alipokea barua hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Wizara
ya Fedha na Mipango, Benny Mwipaja hakuweza kuthibitisha.
Lakini alionyesha kushangazwa kwake
kusikia "barua iliyonakiliwa kwa Waziri Mkuu ipo mitandaoni?"
Mwanzoni mwa wiki iliyopita TRA
ilitangaza kusudio la kupiga mnada kontena 20 za Makonda ikiwa atashindwa
kuzilipia ushuru na kuzichukua ndani ya siku 30 zitakazomalizika katikati ya
mwezi ujao.
Katika tangazo hilo, Kamishna wa Idara
ya Kodi ya Ushuru wa Forodha na Bidhaa, alitoa siku 30 kwa wamiliki wa mali
mbalimbali zilizopo katika ghala la TRA kwenda kuzichukua la sivyo baada ya
muda huo zitapigwa mnada kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa ushuru wa
forodha.



