Waziri Mkuu Atoa Maagizo Mazito kwa Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Awataka Wabadilike

Dar es salaam:
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameziagiza Wizara, mashirika na taasisi zote za Serikali na binafsi zianze
kutumia nishati mbadala ili kuondoa kabisa matumizi ya kuni na mkaa.
“Wizara, taasisi na mashirika yote ya
Serikali na binafsi pamoja na vikundi vya uzalishaji wanaotumia nishati ya kuni
na mkaa kwa ajili ya kupikia au shughuli za uzalishaji waanze kutumia nishati
mbadala ili matumizi ya mkaa yaishe na ikiwezekana yatoweke kabisa,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei
31, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es
Salaam walioshiriki uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye
viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa
ni Gharama: Tumia Nishati Mbadala.”
Waziri Mkuu amesema teknolojia bora
ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo ameiona kwenye maonesho hayo, ikuzwe na
kusambazwa kote nchini ili kuwawezesha wananchi walio wengi waachane na
matumizi ya mkaa wa kawaida na badala yake watumie mkaa-mbadala kwa lengo la
kuhifadhi misitu na kupunguza uharibifu wa mazingira.
Ili kufanikisha matumizi ya
teknolojia hiyo, Waziri Mkuu amesema vibali vya ujenzi wa majengo makubwa na
taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo pia vianze kuzingatia ufungaji wa
mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia ili kurahisisha
upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala katika taasisi na majengo makubwa.
“Wahandisi na wachoraji ramani za majengo
waweke njia za kupitisha kwenye michoro yao ili ujenzi wa nyumba na majengo
haya ukikamilika, watumiaji waweze kutumia teknolojia hiyo,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema
Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike na uachane na matumizi ya mkaa. Kwa
mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani 500,000 za mkaa kwa mwaka.
“Viongozi wa mkoa na wilaya ondokeni
hapa na hili kama ajenda ya mkoa wa Dar es Salaam, mkaifanyie kazi na Wizara
pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi gani. Jitihada zilizofanywa na Jiji la Dar
es Salaam kupitia kwa Mstahiki Meya, za kuanza kuwapa mtaji wajasiriamali hawa
wanaotengeneza teknolojia mpya ni lazima ziigwe na nyie kwenye Manispaa zenu.”
“Meya ametoa fursa na amewaanzishia,
na ninyi sasa endeleeni. Tengenezeni bajeti kupitia Mabaraza ya Madiwani na
muwaunge mkono wajasiriamali wanaotengeneza haya majiko kwa kuwapa teknolojia
hii kwenye maeneo yenu. Wanaotengeneza mashine za mkaa mbadala, wawezeshwe
watengeneze mashine nyingi zaidi na zije kila Manispaa, ili kila Manispaa ianze
kutumia teknonolojia hiyo kupikia,” alisisitiza.
Amewaagiza Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam wafuatilie kwa karibu
usambazaji wa teknolojia hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Yusuf Makamba amesema hali
ya mazingira hapa nchini ni mbaya licha ya kuwa haionekani kwa haraka na watu
waishio mijini.
“Hali ya mazingira nchini mwetu ni
mbaya sana na inawezekana watu wanaoishi Dar es Salaam hawaioni kwa haraka kwa
sababu mahitaji yao yote wanayapata sokoni na madukani,” alisema.
“Wenzetu wa mikoani na vijijii
wanaotegemea mvua na udongo wenye rutuba wanataabika kwa sababu kipato chao
kinaathirika kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema.
Alisema mazingira yanafungamana na
utalii, kilimo, ufugaji, nishati, maji na kwamba maendeleo ya nchi pia
yamefungamana moja kwa moja na mazingira. “Asilimia 90 ya Watanzania wanatumia
kuni na mkaa kupikia lakini asilimia 70 ya mkaa wote unaozalishwa nchini
Tanzania, unatumika jijini Dar es Salaam,” alisema.
Waziri Makamba alisema taasisi za
Serikali kama vyuo, magereza, hospitali na shule zinaongoza kwa matumizi ya
kuni na mkaa na hivyo kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Akitoa mfano, alisema Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM) kina wanafunzi wapatao 30,000 na kinalazimika kuandaa milo mitatu
kila siku.
“Chuo hiki kina migahawa tisa, kule
nyuma kumejaa magogo ya kuni. Kuna mgahawa mmoja mdogo unatumia magunia 17 ya
mkaa kwa siku, sasa huo mkubwa unatumia magunia mangapi?” alihoji.
Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa leo,
yataendelea hadi Juni 5, mwaka huu ambayo ni siku ya kilele. Pia wiki nzima
kutakuwa na makongamano, midahalo na mjadala wa kitaifa.



