Ratiba Nzima Na Makundi Yote Ya Kagame Cup 2018

Wakongwe wa soka Tanzania, Simba SC
na Yanga SC wamepangwa Kundi C katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati, CECAFA Kagame Cup inayotarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu
mjini Dar es Salaam.
Akitaja makundi ya michuano hiyo, Katibu
wa kudumu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA),
Nicholas Musonye alisema kwamba pamoja na Simba na Yanga, timu nyingine katika
Kundi hilo ni Dakadaha ya Somalia na Saint George ya Ethiopia.
Musonye alisema kwamba Kundi A linaundwa
na timu za Azam FC, KCCA ya Uganda, JKU ya Zanzibar na Kator FC wa Sudan
Kusini, wakati Kundi B linaundwa na timu za Rayon Sport ya Rwanda, Gor Mahia ya
Kenya, Lydia Ludic ya Burundi na Ports ya Djibouti. Musonye aliishukuru
Tanzania kwa kukubali kuwa wenyeji wa michuano hiyo na akasema kwamba
anatarajia itafana kwa sababu ya rekodi ya nchi hii kuandaa mashindano
yaliyokuwa na msisimko mkubwa miaka ya nyuma.
Musonye ambaye alisema mashindano
yatafanyika viwanja vya Taifa na Azam Complex, Chamazi – pia amewapongeza
Rwanda na Rais wao, Paul Kagame kwa kuwa wadhamini wa mashindano haya kwa zaidi
ya miongo miwili sasa.
Musonye amesema kwamba wamelazimika
kufanya mashindano ya mwaka huu sambamba na Fainali za Kombe la Dunia nchini
Urusi, kwa sababu wasipofanya mwezi huu hayatafanyika tena kwa mwaka wa tatu
mfululizo.
Hata hivyo, Musonye amesema kwamba
watatoa ratiba nzuri ambayo haitaruhusu mashindano ya mwaka huu kuingiliana na
mechi za Kombe la Dunia.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa
Azam Media Limited, Tido Mhando alisema kwamba wataitumia michuano hiyo
kukizindua kituo chao chao Redio, Uhai FM na akawahakikishia kwamba pamoja na
mashindano hayo kufanyika sambamba na Kombe la Dunia, lakini yatafana
FIFA imeridhia Kagame kufanyika mwezi
huu tofauti na agizo lake la kutotaka katika mwezi wa Fainali za Kombe la Dunia
yasifanyike mashindano mengine yoyote, kwa sababu washiriki watano wa michuano
hiyo wapo kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, ambayo kwa sasa
imesimama kupisha Kombe la Dunia itarejea Julai baada ya kumalizika kwa
michuano hiyo nchini Urusi.
Hao ni KCCA ya Uganda iliyopo Kundi A
katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine nne kwenye Kombe la Shirikisho
ambazo ni Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda, Yanga ya Tanzania
zilizopoi Kundi D zote na Al-Hilal ya Sudan iliyopo Kundi A.
Na kwa sababu hatua ya makundi ya
michuano hiyo ya Afrika itakwenda hadi Agosti, mwezi ambao msimu mpya wa Ligi
Kuu nyingi duniani huanza – michuano ya Kagame isipofanyika mwezi huu kuna
hatari isifanyike tena na mwaka huu kwa mara ya tatu mfululizo.
Azam FC ndiyo mabingwa wa mwisho wa
michuano hiyo ilipofanyika Tanzania, walipowafunga Gor Mahia 2-0 katika fainali
Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya waliokuwa washambuliaji wake
hatari, John Raphael Bocco dakika ya 17 na Muivory Coast, Kipre Herman Tchetche
dakika ya 64.
Na hiyo ndiyo ilikuwa michuano
iliyomtoa mshambuliaji Mkenya, Michael Olunga ambaye kwa sasa anachezea Girona
FC ya Hispania kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China.
Baada ya kufungha mabao matano akiwa
na Gor Mahia na kuibuka mfungaji bora akiwapiku , Osman Bilal Salaheldin wa
Al-Khartoum ya Sudan aliyefunga mabao manne sawa na Tchetche wa Azam FC, Olunga
akachukuliwa na Djurgardens IF ya Sweden mwaka 2016 iliyomuuza Guizhou Zhicheng
mwaka 2017.
Na Tanzania itawakilishwa na Azam FC
kama mabingwa watetezi wa mashindano na Yanga SC, kama mabingwa wa nchi.
Credit: Full Shangwe



