Breaking News

Profesa Ndalichako: Serikali Inatambua Mchango wa Sekta Binafsi Katika Kuboresha Elimu Nchini.

WAZIRI wa elimu sayansi na teknolojia  Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali ya Tanzania inatambua mchango wa sekta binafsi   katika kuboresha sekta ya elimu nchini kwa lengo la kutimiza azma ya Serikali kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora.

Akizungumza jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa shule ya Turkish maarif iliyopo boko alisema serikali ya awamu tano pamoja na hatua mbalimbali ambazo imekuwa ikizichukua kuboresha elimu nchini inatambua mchango mkubwa wa wadau na hatua ambazo wamekuwa wakizichukua kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya elimu nchini. 

"Ndugu zetu kupitia taasisi yao ya Turkey maarif Foundation tunatambua sekta ya elimu ni muhimu sana katika taifa letu hivyo tunawahamasisha kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine mfano Dodoma," alisema Profesa Ndalichako

Alisema nchi ya uturuki na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu hususani uwekezaji katika sekta ya elimu na natoa pongezi kwa hatua ya kujenga shule katika katika mkoa wa Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na kuwakaribisha kujenga katika mkoa wa Dodoma .

Aidha Profesa Ndalichako aliongeza kuwa serikali imekuwa ikitoa  kipaumbele katika sekta ya elimu (bila malipo) kwa kutoa kila mwezi kiasi cha zaidi bilioni 28 ili kuboresha sekta ya elimu nchini kama nyenzo muhimu ya kufikia uchumi wa kati.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi balozi wa uturuki nchini Tanzania Ali Davutoglu alisema wameamua kujenga shule hizo nchini Tanzania kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na uturuki na amani iliyopo nchini na kwamba shule ni kwa lengo la kuimarisha elimu na kuboresha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

"Shule hii tunayoizindua leo itahudumia wanafunzi 600 Tarkish maarif ni moja ya shule maarufu hapa Tanzania zenye takriban wanafunzi 1900" alisema Davutoglu.