Uzinduzi wa Wiki ya Wawekezaji, Tahadhari Yatolewa kwa Matangazo Holela Mitandaoni.

Wito umetolewa kwa wawekezaji na Umma kuwa makini na fursa za uwekezaji zinazotangazwa kiholela kwa njia ya mitandao ambazo hazijaidhinishwa na mamlaka husika za usimamizi wa uwekezaji.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama katika uzinduzi wa wiki ya wawekezaji katika Masoko ya Mitaji Duniani.
CPA Mkama amesema CMSA inaadhimisha wiki hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya masoko ya mitaji kuendesha kampeni ya kutoa elimu kwa makundi mbalimbali na umma kuanzia oktoba 5 hadi 9 mwaka huu ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masoko ya mitaji na uwekezaji.
Aidha amesema uzinduzi huo ni sehemu ya utekekelezaji wa mpango mkakati wa CMSA wa miaka mitano 2018/19 hadi 2022/23 ambao unapanga kuendeleza sekta ya masoko ya Mitaji Tanzania kwa kutoa elimu na kuongeza uelewa kwa makundi mbalimbali na kupanua wigo wa washiriki na kujenga uwezo kwa watendaji katika masoko ya mitaji kulinda maslahi ya wawekezaji.
Hata hivyo amesema kwa kuzingatia kuwa Tanzania inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda mahitaji ya mitaji kwa shughuli za uchumi yanaongezeka hivyo ni vyema kujenga uwezo na ushirikiano wa pamoja na wadau wakuu wa sekta ya masoko ya mitaji utawezesha wahitaji mitaji ya kifedha.
Sambamba na hayo amesema mpaka sasa uwekezaji katika masoko ya mitaji ni shilingi Trilioni 27 ambapo uwekezaji katika hisa ni Trilioni 15 Hati fungani Trilioni 11.5 na mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni bilioni 500.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mifuko ya uwekezaji wa pamoja (UTT-AMIS) Simon Migangala amesema kwa miaka michache uwekezaji umeongezeka hadi kufikia wawekezaji elfu 12 ambapo ukuaji ulikuwa haujazidi Milioni 22 na sasa ukuaji umefika hadi milioni 122.




