Breaking News

TBS YAWATAKA WASAFIRISHAJI BIDHAA NJE YA NCHI KUZINGATIA VIWANGO.

Wauzaji wa bidhaa za nje ya nchi wameshauriwa kuhakikisha bidhaa zao zimekaguliwa na kukidhi viwango na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuepuka usumbufu wanaposafirisha bidhaa hizo.

Ushauri huo umetolewa jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw. David Ndibalema wakati akifungua Mkutano wa wasafirishaji wa bidhaa za nje ya nchi. 

Alisema cheti cha ukaguzi wa ubora wa bidhaa kinachotolewa na TBS kinatambulika kwa nchi mbalimbali hivyo kutia wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa zao zimekaguliwa na kupatiwa cheti cha ubora ili kusiwe na changamoto za kukwama katika nchi za wenzetu.

"Kuna wasafirishaji ukwama pindi wanaposafirisha bidhaa zao nje ya nchi wakiombwa cheti cha ubora wa bidhaa zao hivyo kushindwa kusaidika kutokana kutokuwa na ufahamu majukumu ya TBS". Alisema Bw. Ndibalema.
Alisema dhumuni ya kuandaliwa kwa semina hiyo kutoa elimu kwa wasafirishaji na wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa zao nje ya nchi kutambua majukumu na huduma zinazotolewa na Shirika hilo.

Aidha Ndibalema ameongeza kuwa semina hiyo imejikita zaidi kuwajengea uelewa namna Wizara na Taasisi nyingine zinavyo shirikiana na wasafirishaji wa bidhaa za mazao ya kilimo, chakula kwenda nje ya nchi sambamba na kujadiliana juu ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo hususani kwenye usafirishaji wa bidhaa.