Breaking News

TMA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA KUWA ZA WASTANI HADI JUU YA WASTANI

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  (TMA) imesema katika kipindi cha Mvua za Masika Mwezi Machi mpaka Mei mwaka huu mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Akizungumza jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirikisho la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt Agness Kijazi wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa msimu wa mvua za masika Mwezi Machi mpaka Mei mwaka huu alisema  mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari na kuisha mwezi Mei mwaka huu katika maeneo mbalimbali nchini.

Dkt Kijazi amesema ongezeko la mvua hizo linatarajiwa hasa katika kipindi cha Mwezi Machi katika maeneo ya pwani ya Kaskazini na Mwezi April kwa maeneo ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki.

‘Msimu wa mvua za Masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita,Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma’amesema Dkt Kijazi
Amesema katika Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani na kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari, 2022. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha katika wiki ya tatu ya mwezi Mei, 2022.

Aidha Mkurugenzi huyo amezitaja athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua hizo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na usalama wa chakula kuwa vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji a baadhi ya mazao yasiyohitaji maji mengi.

‘Katika sekta ya Afya Kutokana na mvua zinazotarajiwa, upo uwezekano wa kuongezeka kwa athari za magonjwa ya kuambukiza, hususan magonjwa yatokanayo na wadudu-dhurifu na matumizi ya maji yasiyo salama kwa afya. Hivyo, mamlaka husika zinashauriwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kutosha katika vituo vya kutolea huduma za afya mapema, kwa kuzingatia uwezekano wa uharibifu wa miundombinu unaoweza kujitokeza hususan katika vipindi vya mvua kubwa. Jamii inasisitizwa kuchukua hatua kwa kuhakikisha usafi wa mazingira yanayowazunguka, kuharibu mazalia ya mbu, kudumisha usafi kwa ujumla’ameendelea Dkt Kijazi

Awali akitoa tathmini ya mwenendo wa mvua za vuli kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2021Mtaalamu wa Hali ya Hewa  Rose Senyagwa amesema kuwa TMA ilitoa utabiri wa uwepo wa mvua za wastani hadi chini ya wastani ambapo kiwango cha usahihi wa utabiri kilikuwa cha  asilimia 93.8.

Hata hivyo  Mamlaka hiyo imewashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima,wafugaji,mamlaka za wanyamapori,wasafirishaji,mamlaka za maji na afya kuendelea kutafuta,kupata na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika sekta husika