Breaking News

LHRC: JAMII KEMEENI MILA POTOFU NA VITENDO VYA UNYANYASAJI WA KIJINSIA

Kituo cha Sheria na haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka jamii kukemea na kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zimekiwa zikikandamiza ustawi wa wanawake pamoja na kutofumbia macho vitendo vyovyote vya kikatili dhidi yao.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga wakati akitoa tamko la siku ya Wanawake Duniani.

Aidha amewataka wanawake kujiamini kuwa wanaweza kuwa yeyote wanaetaka kuwa bila kuruhusu jamii kuwatafsiri uwezo wao bali wazikimbize ndoto zao kwa kutumia fursa zilizopo na kujiendeleza kielimu.

Hata hivyo amezitaja changamoto ambazo bado zinawakabili wanawake ikiwemo ukatili, sheria za Tanzania bado zinamkandamiza mwanamke, uhuru wa kiuchumi, upatikanaji wa elimu, mila na desturi zilizopitwa na wakati, kutokuwa na usawa wa kijinsia na uongozi ngazi za maamuzi.

Sambamba na hayo LHRC imependekeza uwepo wa mipango madhubuti yenye bajeti ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa, kuimarisha huduma za jamii, utoaji elimu, uwepo wa sheria mahususi za ukatili wa kijinsia pamoja na kuhakikisha serikali inajumuisha jinsia katika programu zake.

Mbali na hayo ameyataja mafanikio ya Tanzania katika mabadiliko mbalimbali katika masuala ya uongozi toka mwaka 1997 ni pamoja na teuzi mbalimbali za wanawake nafasi za ukurugenzi serikaliza mitaa 52 dhidi ya 132, uwaziri toka nafasi 4 hadi 9 dhidi ya 16, mabalozi 9 dhidi ya 33 na wakuu wa mikoa 6 dhidi ya 20.