NCCR MAGEUZI KUSHIRIKI MKUTANO NA RAIS SAMIA
Chama cha NCCR-Mageuzi, kimekubali kushiriki mkutano wa majadiliano ya amani ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), unaotarajiwa kufanyika jijini Dodoma tarehe 30 hadi 31, Machi 2022, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza makao makuu ya chama hicho jijini Dar es salaam, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma Taifa, Edward Simbeye juu ya maadhimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, iliyoketi march 9 jijini Dar es salaam.
Alisema, Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi imetengua uamuzi wake wa kutoshiriki mkutano huo, baada ya mapendekezo yake ya kukutana na Rais Samia kabla ya mkutano huo, kufanyiwa kazi.
Sembeye aliongeza kuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, atakiwakilisha chama hicho katika mkutano huo, uliotishwa kwa ajili ya kutafuta tiba ya majeraha ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.
“Tulisema kama hilo halitafanyika basi hatutakuwa na radhi kwenda kwenye mkutano huo sababu sisi hatuamini katika unafiki, tunaamini katika kweli, tuzungumze tutibiane makovu ya uchaguzi, tuzungumze uso kwa uso kabla ya kwenda kwa umma, hilo limezingatiwa,” alisema Simbeye.
Alisema, kwa kuwa pendekezo lao hilo limekubaliwa, chama hicho hakina sababu ya kutoshiriki mkutano huo wa TCD na Rais Samia.
Aidha sembeye alibainisha kuwa chama cha NCCR-Mageuzi kinahitaji muafaka wa kitaifa na Tanzania iliyo salama na yenye amani .
“Tunataka kila mtu apate haki yake, ndiyo maana tulikuwa tunasimamia haki. Pale ambapo kuna haki tunasimamia haki, pale ambapo hakuna haki hatutakuwa wavivu kusema hapa hakuna haki na tutatoa njia ya kupata haki,” alisema Simbeye
“Ndiyo maana tumekubaliana kwamba kuna mwanga wa kushirki mkutano huu na baada ya hapo majadiliano mengine yataendelea.



