SERIKALI MBIONI KUZALISHA WATAALAMU WA KIDIGITALI – DKT. MUNISI
Dar es Salaam - Serikali imeeleza kuwa inaendelea kuwekeza katika ukuzaji wa rasilimali watu ili kuzalisha wataalamu wa kidijitali wa kutosha nchini, hatua itakayopunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi katika miaka ijayo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Dkt. Evaline Munisi, alipotembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Dkt. Munisi alisema Serikali pia inaendelea kusimamia ustawi wa wafanyakazi kwa kuhakikisha maeneo ya kazi yanazingatia viwango vya chini vya mishahara na haki nyingine za wafanyakazi.
Alisema kupitia uwekezaji unaofanyika katika sekta mbalimbali, Tanzania itaendelea kuzalisha wataalamu wa kidijitali wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira nchini.
"Baada ya miaka kadhaa hatutakuwa na wataalamu wa kidijitali kutoka nje ya nchi, kwa sababu tunawaandaa na kuwazalisha wenyewe kupitia sekta mbalimbali nchini," alisema Dkt. Munisi.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kudumisha mahusiano mema sehemu za kazi na katika jamii kwa kuwa yanachangia kuimarisha uzalishaji na kukuza uchumi wa taifa.
"Sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) tunapenda kuona kuna mahusiano mazuri na jamii, kwa kuwa kupitia mahusiano hayo tunapata maendeleo. Hivyo nitoe rai kwa jamii kuendelea kudumisha mahusiano mazuri ili kukuza uchumi wa nchi," alisema.
Katika ziara yake kwenye maonesho hayo, Dkt. Munisi alitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zikiwemo WCF, OSHA na NSSF, ambapo alipata fursa ya kujionea huduma na elimu vinavyotolewa kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo.




