MADINI YATAJENGA UCHUMI WA TANZANIA KUELEKEA DIRA YA TAIFA 2050 – DKT. SHINGO
Dar es Salaam – Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Reuben Leka Shango, amewahimiza Watanzania kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba 2026, Dkt. Shango amesema banda la Tume ya Madini linatoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli zote za madini kuanzia utafiti, utoaji wa leseni, uchimbaji, masoko, uongezaji thamani wa madini hadi fursa za uwekezaji na utoaji wa huduma katika sekta hiyo.
Amesema wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata ufahamu wa namna ya kushiriki kisheria katika shughuli za madini, ikiwemo taratibu za kupata leseni na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sekta hiyo nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Shango, sekta ya madini ina nafasi kubwa ya kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa zilizopo kama wachimbaji, watafiti, watoa huduma, wafanyabiashara wa madini na wawekezaji katika shughuli za uongezaji thamani.
Aidha, amewapongeza waandaaji wa Maonesho ya Sabasaba kwa kuendelea kutoa jukwaa linalowawezesha taasisi za umma na binafsi kuonesha bidhaa, huduma na fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wananchi.
Dkt. Shango pia amewaalika wananchi kutembelea Kijiji cha Madini kilichopo ndani ya maonesho hayo ili kupata elimu na kujionea fursa zinazopatikana katika sekta ya madini.




