Breaking News

SERIKALI KUONGEZA KASI YA KUSAMBAZA UMEME MAENEO YA MIGODI

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashengo, ametembelea Banda la Wizara ya Nishati katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ambapo amepatiwa taarifa kuhusu hatua za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa umeme kwenye maeneo ya migodi.

Akiwa katika banda hilo, Dkt. Lekashengo ameelezwa kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme katika maeneo ya migodi ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuchochea maendeleo ya sekta ya madini.
Miongoni mwa maeneo yanayonufaika na mpango huo ni migodi midogo iliyopo Chunya mkoani Mbeya na Msisi wilayani Handeni, mkoani Tanga, ambako Serikali inaendelea kuwezesha uunganishaji wa umeme kwa wachimbaji wadogo.

Ziara ya Dkt. Lekashengo ni sehemu ya mwendelezo wa viongozi mbalimbali wanaotembelea Banda la Wizara ya Nishati kujionea mafanikio na mipango ya Serikali katika kuboresha huduma za nishati nchini kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba.