Breaking News

ACT-WAZALENDO YACHAMBUA RIPOTI YA CAG 2020/2021

Kiongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe akizungumza wakati wa wasilisho la uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia mwezi Juni 2021 April jijini Dar es Salaam.
Waziri Kivuli, Fedha na Uchumi wa Chama Cha ACT-Wazalendo Emmanuel Mvula akiwasilisha uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia mwezi Juni 2021 jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam:
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimefanya uchambuzi wa mambo 10 kuhusu Ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia mwezi Juni 2021.

Akiwasilisha uchambuzi huo leo Aprili 14, 2022 jijini Dar es Salaam Waziri Kivuli, Fedha na Uchumi wa chama hicho Emmanuel Mvula amesema kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, thamani ya jumla ya hoja za ukaguzi katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ujumla wake na kwa ripoti zote tatu kuu za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma ni Shilingi trilioni 5.8.

“….ikilinganishwa na mwaka 2019/2020 kwa ujumla wake thamani ya hoja za ukaguzi ilikuwa ni Shilingi Trilioni 3.6 na Dola za Marekani Milioni 596,”.

Mvula ameainisha mambo hayo kuwa ni pamoja na, Fedha kutumiwa bila kupita Mfuko Mkuu wa Hazina limekuwa tatizo sugu.

Kwamba katika mwaka 2020/2021 jumla ya matumizi yenye thamani ya shilingi trilioni 1.2 yalifanyika bila kupita Mfuko Mkuu.

“Matumizi ya fedha za Serikali bila kupita kwenye Mfuko wa Hazina ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi yetu Ibara ya 135(1) ambayo inaelekeza kuwa ni lazima kila fedha ya Serikali itunzwe kwanza kwenye Mfuko Mkuu kabla ya kutumika na kuidhinishwa na CAG,” amesema Mvula.

Madai ya Watumishi wa Umma Shilingi Bilioni 429

Waziri huyo Kivuli amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka saba sasa watumishi wa umma wa Tanzania hawajapandishiwa mishahara licha ya gharama za maisha kuongezeka kwa kasi kubwa.

Ameeleza kwamba kwa mujibu wa Kanuni Na. 23 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma ya mwaka 2009, madai ya Watumishi yanatakiwa yalipwe mara tu yanapotokea.

“Hata hivyo, CAG ameonyesha kuwa madai yanayotokana na watumishi kutokulipwa kwa wakati, malimbikizo ya mishahara ya waajiriwa wapya na waliopandishwa madaraja, makato na posho za watumishi yamefikia shilingi bilioni 429. Ripoti ya CAG ya 2020/21 inaonyesha kuongezeka kwa madai haya kutoka Sh. bilioni 334.15 kwa mwaka wa fedha 2019/20 hadi Sh. bilioni 429.80 kwa mwaka huu wa ukaguzi  ni sawa na ongezeko la 28%,” amebainisha Mvula.

Hivyo ameitaka Serikali iwalipe watumishi malimbikizo ya madai yao mara moja na kwa mkupuo.

Madai ya Wazabuni kwa Serikali yafikia Shilingi Trilioni 3.6

Amesema uchambuzi wao umebaini kwamba, mwaka 2020/2021 madai ya wazabuni kwa Serikali (accumulated libalities OR Payables) yalikuwa na jumla ya Shilingi Trilioni 3.6 kutoka Shilingi Trilioni 3.1 mwaka 2019/20.

“Madai ya Wazabuni dhidi ya Serikali yaliongezeka kwa shilingi bilioni 500 kutoka mwaka uliopita. Hiki ni kiwango kikubwa sana cha Fedha za watu ambazo Serikali inazishikilia mkononi baada ya kupokea huduma za Wazabuni hao. Hali hii inasababisha mdororo wa uchumi, kwani Serikali inashikilia Fedha za wakandarasi, wafanyabiashara na watoa huduma na hivyo kudumaza shughuli za uzalishaji mali, na wakati mwingine kufukarisha wananchi,” ameeleza. 

Ubadhirifu wa Shilingi Bilioni 279.5 katika miradi mbalimbali

Amebainisha katika uchambuzi wao wamebaini ubadhirifu wa thamani ya shilingi bilioni 279.5 kutoka katika miradi mitatu ambayo ni mradi wa ujenzi wa vihenge vya NFRA kuhifadhia chakula.

Amesema CAG katika ripoti yake amefanya ukaguzi kuhusu mradi huo ambao ulipaswa kukamilika mwaka 2017 na muda wa kukamilika ulisogezwa mbele mpaka Disemba 2020 lakini mradi huo haujakamilika.

Kwamba kwa mujibu wa CAG wakandarasi wawili walipewa kazi, mmoja ya kukarabati maghala yaliyopo sasa, kampuni ya UNIA SP.2.00 kutoka Poland na Mkandarasi mwengine ni Kampuni ya FERRUM SA kutoka huko huko Poland.

“Mradi mzima uligharimu jumla ya shilingi Bilioni 134.2 na wakandarasi walilipwa 65% ya fedha zote za mradi. Mradi huu haujakamilika mpaka leo na CAG alipotembelea maeneo ya mradi hapakuwa na dalili yeyote ya shughuli za mkandarasi. Kiufupi, kama Taifa tumepigwa shilingi bilioni 87.2 na hakuna vihenge wala maghala,”.

Hivyo  ameitaka Serikali iwasiliane na Ubalozi wa Poland nchini ili kuwapata wakandarasi hawa na hatua stahiki kuchukuliwa na kuhakikisha mradi unakamilika.

Ubadhirifu mwingine ni kwenye bandari ya Tanga ambapo ameeleza kwamba hii imetokana na “Mkandarasi Mkuu” aliyepewa kazi na Mamlaka ya Bandari kumpa kazi hiyo “Mkandarasi Mbia” kwa gharama ya chini na hivyo mkandarasi wa kwanza kupata faida ya shilingi bilioni 64.3 bila ya kufanya kazi.

Mvula amebainisha ubadhirifu mwingine ni katika mradi wa Mkulazi bilioni 128.3 ambapo mwaka 2019, TANROADS iliingia mkataba kinyume na utaratibu na sheria za nchi.

Kwamba mkataba huo uliipa TANROADS mamlaka ya kusanifu, kuleta, kusimika na kuzindua mtambo wa kiwanda uliogharimu jumla ya shilingi bilioni 128.3.

“CAG alibaini mkataba huu haukuwa na vielelezo vya uhakiki wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama inavyotakiwa na kanuni ya 59 (1) ya kanuni ya manunuzi ya umma ya mwaka 2013. Aidha, kampuni ya Mkulazi haikuwa na jukumu la kusimamia mkataba huo kutokana na makubaliano ya awali kufanyiwa marekebisho na kuipa TANROADS mamlaka ya kusaini mkataba na kusimamia mradi huo,”.

Kwamba kiutaratibu, malipo kwa ajili hiyo hufanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa sekta Binafsi baada ya kupokea hati na nyaraka za malipo kutoka kwa wakala wa barabara. Kutofuatwa kwa taratibu za manunuzi kulisababishwa na kukosekana kwa uwazi katika maandalizi ya zabuni, kuomba, tathmini na kutoa zabuni kunakoweza kusababisha hatari, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mitambo isiyokidhi viwango vinavyotakiwa, kununua mtambo kwa bei kubwa, kuchelewa kuletwa kwa mitambo uliionunuliwa na hivyo kushindwa kupata thamani ya fedha katika mkataba huo.

Kuvunja mikataba kiholela, kumesababisha nchi kupata hasara ya shilingi bilioni 478

Amesema katika mwaka wa fedha 2020/21, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Idara ya Jeshi la Magereza walikatisha mikataba mitatu yenye thamani ya Sh. bilioni 126.55 kutokana na wakandarasi hao kutofanya kazi vizuri.

Pia, amesema ripoti ya CAG kwenye Mashirika ya Umma imeonekana kuwa Serikali imebidi kuilipa kampuni ya symbion jumla ya dola za Marekani milioni 153.4 sawa na shilingi bilioni 352, kutokana na kitendo cha kuvunja mkataba wa kufua umeme na kampuni hiyo bila ya kufuata taratibu.

Hivyo ameitaka Serikali kuheshimu mikataba na kufuata taratibu za sheria kama inatakiwa kusitisha mikataba husika ili kuepeuka hasara kama hizi na Taasisi za Serikali ziepuke kufanya maamuzi bila kwanza kupata ushauri wa kisheria wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wizi mkubwa wa Shilingi Bilioni 71 Mamlaka ya Bandari Tanzania

Amesema CAG alifanya ukaguzi maalumu katika Mamlaka ya Bandari Tanzania na kubaini ubadhirifu wenye thamani ya shilingi Bilioni 71.

Kwamba ubadhirifu huu ulihusisha haswa Bandari ya Mwanza na Bandari ya Dar es Salaam ambapo fedha za umma zilikuwa zinahamishwa kupelekwa Mwanza na kutumiwa bila kufuata taratibu.

“Katika ukaguzi huo CAG hakuona ushahidi wa maombi ya kuhamisha fedha shilingi bilioni 22.6 zilizotumwa kwenda Mwanza. Pia, kukosekana kwa ushahidi wa idhini ya kuhamisha fedha Shilingi Bilioni 24.29 zilizotumwa Bandari ya Mwanza Kati ya miamala 157 ya kuhamisha fedha,” amesema.

Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere

Mvula amesema katika Ripoti ya Mwaka huu pia CAG ametoa hoja za ukaguzi kuhusu Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere kama ilivyokuwa kwa mwaka jana.

Kwamba CAG amesema katika Taarifa yake kuwa kucheleweshwa kwa ukamilishwaji wa mradi kutaligharimu zaidi taifa (kuongeza muda wa utekelezaji na fedha kwa wakandarasi na washauri) kwani taarifa za CAG zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 48.02 hadi Disemba 2021 tofauti na matarajio ambayo ilitakiwa kufikiwa asilimia 94.7.

“ACT Wazalendo inawashauri wabunge na madiwani kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa zinazoguswa na Mradi wa Bwawa la Nyerere wakutane na Mkandarasi kuweka makubaliano ya namna zitakavyolipwa Fedha zao ili waweze kutekeleza masuala ya maendeleo katika maeneo yao. Vile vile tunaitaka Serikali kufanya marejeo ya mradi huu na kupendekeza namna bora zaidi za kuutekeleza ili kuwa na manufaa kwa nchi yetu,”.

Madai na Madeni ya Mashirika ya Umma

Ameeleza kuwa katika Mashirika ya Umma 200 aliyoyakagua CAG, mashirika 45 ni ya biashara na yaliyosalia ni ya huduma. Vile vile ameeleza kuwa Serikali ilitoa ruzuku ya jumla ya Shilingi trilioni 5.9 kwa Mashirika ya Umma. 

Kwamba CAG pia ameonyesha mashaka yake makubwa katika suala zima la ukusanyaji duni wa madai ya Mashirika ya umma uliopelekea kuwa na madai kwa mashirika 93 kiasi cha shilingi Trilioni 3.71 na hivyo kuchelewesha maendeleo ya mashirika hayo katika kuchochea ukuaji wake na ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Madai ya shilingi trilioni 3.4 ya mashirika ni kwa mashirika mengine ambapo kampuni binafsi kiasi cha Sh. Trilioni 1.45 na mashirika ya Serikali kiasi cha Shilingi Trilioni 1.97. Madai haya yanaathiri mtiririko wa fedha katika taasisi hizi, na hivyo kusababisha kutotekelezwa kwa shughuli zilizopangwa za mashirika yenyewe.

Hivyo amependekeza kuwa Taasisi za Serikali zinazodaiwa na Mashirika ya Umma zilipe na kumaliza madai haya mara moja.

 Mchwa wamejaa tele Serikali za Mitaa

Amesema wamebaini moja wapo ya chanzo cha hasara katika Halmashauri nchini zinatokana na uwepo wa mianya na udhaifu katika mifumo iliyowekwa kuratibu makusanyo ya mapato ya Halmashauri kupitia mawakala, watumishi na mashine za kukusanyia mapato, POS.

Ameeleza, baadhi ya watumishi na mawakala wamekuwa wakitumia mbinu za udanganyifu, kinyume na utaratibu na mifumo ya ukusanyaji mapato kwa mbinu za kughushi stakabadhi, kutokuwasilisha mapato kwa njia rasmi na kutumia njia za dirisha la nyuma kufanya makusanyo.

Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam – Manispaa ya Ilala, ilipata hasara ya Bilioni 10.3 ambazo hazikuwasilishwa na mawakala na watumishi kwenye Halmashauri. Watumishi na Mawakala hao walitumia mbinu ya kubadili taarifa za mfumo wa kutoa stakabadhi,” amesema na kuongeza.

“ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa Serikali ichukue hatua kali kwa watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa upotevu mkubwa wa mapato ambao umetokana na wizi kupitia mashine za kukusanya mapato. Vile vile Serikali iimarishe mfumo wa makusanyo ili kuziba mianya kama hii nchi nzima,”.

Hali mbaya ya kifedha ya Mifuko ya PSSSF na NSSF

Amebainisha, katika uchambuzi wamebaini kuwa kwa mwaka 2020/21 mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) ulilipa gharama za mafao pensheni kuzidi mapato ya michango kwa shilingi bilioni 767.