ALIYEPANDIKIZWA FIGO HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI ATOA VYETI VYA SHUKRANI KWA MADAKTARI BINGWA WALIOFANIKISHA MATIBABU YAKE
Bw. Samwel Kishosha akishuhudiwa na mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru (katikati) akikabidhi vyeti kwa madaktari bingwa wa wa Figo waliomsaidia katika mchakato wa matibabu yake ikiwa ni kuonyesha shukrani kwa madaktari hao na jamii nzima ya Hospitali.
Na Mwandishi Wetu
Bw. Samwel Kishosha ambaye alipandikizwa Figo Hospitali ya Taifa Muhimbili mwezi Machi mwaka huu, ametoa vyeti vya shukrani kwa Madaktari Bingwa wa Figo waliomsaidia katika mchakato wa matibabu yake ikiwa ni kuonyesha shukrani kwa madaktari hao na jamii nzima ya Hospitali.
Bwana Kishosha ambaye alikuwa anakabiliwa na tatizo la Figo zote mbili kushindwa kufanya kazi amesema vyeti hivyo haviwezi kufikia thamani ya huduma aliyoipata isipokuwa ni ishara ya moyo wa shukrani.
“Nimepitia kwenye matibabu ya kuchuja damu (Dialysis) kwa miaka mitatu, matibabu haya yalinigharibu pesa nyingi kwa kuwa ilitakiwa nilipie TZS 320,000 mara tatu kwa kila wiki, nilitaka kwenda India kufuata matibabu lakini nilifika nilikuta India ipo hapa” amesema Bw. Kishosha ambaye ni afisa wa Benki ya CRDB
Anasema changamoto kubwa aliyoipitia wakati wa mchakato wa kupandikizwa ilikuwa ni namna ya kupata ndugu wa kujitolea figo ambapo wengi hawakuwa tayari kufanya hivyo kwa kuhofia vitu mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru alimpongeza Bw. Kishosha kwa kuonyesha moyo wa shukrani na amesema kwamba uanzishwaji wa huduma mbalimbali za kibingwa ndio shabaha kubwa ya hospitali.
“Utoaji wa huduma bora za kibingwa ndio kipaumbele cha Hospitali na hii imetokana na uwekezaji mkubwa ambao serikali za awamu mbalimbali umeufanya kwa kusomesha wataalamu na kununua vifaa tiba ili kuhakikisha huduma kama hizi za upandikizaji wa Figo zinapatikana nchini ili kuwapa wananchi unafuu tofauti na awali ambapo ilibidi wazifuate nje ya nchi kwa gharama kubwa” amesema Prof. Museru
Prof. Museru amesema toka huduma za upandikizaji figo zianzishwe Muhimbili jumla ya wagonjwa 70 wameshapandikizwa.
Ametaja huduma nyingine za kibingwa ambazo MNH imeanzisha kuwa ni pamoja na upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia pamoja na tiba radiolojia
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Figo Dkt. Jonathan Mngumi amemshukuru Bw. Kishosha kwa moyo wake wa shukrani kwa kuwa siyo watu wote wana moyo huo.





