Breaking News

CHADEMA JIMBO LA KAWE YAISHAURI SERIKALI KUINGILIA KATI KUPANDA GHARAMA ZA MAISHA

Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam, bw. Leonard Manyama ameishauri Serikali kuchukua hatua kutokana na kupanda gharama za maisha ili kuwapatia ahueni wananchi.

Manyama alisema serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kutokana na upandaji wa gharama za maisha hususan nauli na mafuta badala ya kuishia kutaja chanzo ni vita kati ya Urusi na Ukraine.

“Wote ni mashahidi Kumekuwepo na kupanda kwa gharama za maisha kila kukicha, nauli na mafuta yamepanda bei, huku serikali ikisema chanzo ni mgogoro kati ya Urusi na Ukraine sasa vita vya Ukraine vimeingiaje,” Alisema Manyama.

Alisema chanzo cha kupanda kwa gharama hizo kunatokana na kodi zilizoongezwa na Serikali kwenye baadhi ya maeneo yakiwemo ya Barabara, TARURA ambazo jumla shilingi 513.

Manyama ameitaka Serikali kuangalia suala hilo kwa maslahi mapana ya kuwasaidia wananchi kwani hakuna ulazima wa kuongeza kodi hizo kipindi hiki ambacho gharama za maisha zimezidi kuwa juu.

Aidha ameomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa shilingi 513 katika maeneo hayo ili uchumi upumue na kuwapa ahueni wananchi.

“Chadema Jimbo la Kawe, Tunaishauri serikali kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na tatizo hilo kwa kuziondoa kodi hizo kwa sasa ili wananchi watuliwe mzigo huu,” amesema Manyama.

Amesema kupanda kwa bei ya mafuta kumesababisha pia kupanda kwa bidhaa nyingine, hivyo kusisitiza Serikali kuchukua hatua madhubuti.

Akizungumzia kuhusu suala la mishahara ya watumishi wa umma, ameitaka Serikali kuwapandisha mishahara yao kwani imepita miaka sita bila kupandishwa.

Manyama katika hilo, amelitaka shirikisho na wafanyakazi pamoja na TUCTA kutekeleza majukumu yao kwa kutetea na kudai maslahi ya wafanyakazi.