RC MAKALLA AAMURU KUKAMATWA VINARA WA UUZAJI ARDHI MTAA WA MBONDOLE MSONGOLA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla ameamuru kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mbondole na Wajumbe kwa tuhuma za kushiriki utapeli wa kuuza eneo la Mwananchi kwa Wavamizi zaidi ya 700 ambao mpaka Sasa hawajui hatma yao Baada ya Mahakama kuamuru nyumba zaidi ya 200 za Wavamizi zivunjwe.
RC Makalla ametoa maamuzi hayo wakati alipotembelea eneo Hilo na kujionea Hali halisi Kisha kufanya mkutano wa hadhara uliokutanisha Mmiliki halali wa eneo na Wavamizi na kutoa maelekezo ya kuzingatiwa wakati Suluhu ikitafutwa.
Miongoni mwa maelekezo aliyotoa RC Makalla ni pamoja na kusitishwa kwa Shughuli yoyote ya mauziano ya Ardhi na uendelezwaji wowote wa Ardhi mpaka pale Serikali itakapotoa maelekezo.
Aidha RC Makalla ameelekeza TAKUKURU kufanya mapitio ya Nyaraka zote za mauzioano ili ipatikane taarifa kamili na wote waliohusika wawajibishwe kwa mujibu wa sheria ambapo amekemea Vitendo vya uvamizi wa maeneo na uuzaji Ardhi kiholela.
Pamoja na hayo RC Makalla
amesema Baada ya kupatikana kwa taarifa kamili Serikali itakaa meza moja na Mmiliki, Wawakilishi wa Wavamizi na Kamati ili kutoka na muafaka wa pamoja wa kumaliza Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 10.
Katika mkutano wa Leo RC Makalla kwa kushirikiana na Wataalamu wamepitia nakala zaidi ya 108 za mauziano ya zaidi ya Shilingi Milioni 179 ambapo kiasi chote hicho Cha fedha kimeliwa na "wajanja".








