Breaking News

BENJAMINI MKAPA FOUNDATION KUFANYA KONGAMANO LA PILI 13 JULAI ZANZIBAR

TAASISI ya Benjamin William Mkapa Foundation (BMF) kwa ushirikiano na Serikali imepanga kufanya jukwaa la kumbukizi ya pili ya aliyoyafanya na kuacha alama muasisi wa Taasisi ambaye pia alikuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Ellen Senkoro amesema jukwaa hilo la siku mbili litafanyika Zanzibar, Julai 13 hadi 14 mwaka huu.

“Kauli mbiu ya jukwaa hili ni ‘Uongozi Madhubuti Hamasa ya Mabadiliko kwa Wote’ (Resilient Leadership-Inspiring Change for All). Ka siku hizo pia kutakuwa na mdahalo kuhusu mada kuu mbili,” amesema Dkt. Senkoro.

Amezitaja mada hizo kuwa ni kuongea kasi katika mikakati ya Mabadiliko katika mifumo ya afya Tanzania kupitia biashara ushirika (Accelerating Strategic Health Transformation in Tanzania through Business Coalition.

Nyingine ni ubunifu katika Miradi na mikakati ya Kati ya Serikali, Taasisi za umma na za binafsi katika kuleta huduma ya afya kwa Wote. (Innovative Public-Private Partnerships (PPP) approaches towards attaining Universal Health Coverage).

Kwamba kupitia mada hizo washiriki watapata fursa ya kusikia mijadala ya juhudi za mashirikiano ya Serikali za Tanzania Bara na Visiwani, Sekta binafsi na wadau wa maendeleo na pia iliyoendelea kuchagizwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa, katika kuimarisha mifumo ya afya kwa lengo la kuhakikisha kila mtu popote alipo anapata fursa ya kupata huduma bora za afya.

Dkt. Senkoro amesema mjadala huo pamoja na mambo mengine utashirikisha jopo la wadau watakao chambua kwa undani umuhimu wa biashara na uwekezaji wa pamoja katika kuinua afya na ustawi wa kila mmoja Wetu.

“Mdahalo huu wa Siku mbili utaanza saa mbili asubuhi na unatarajia kumalizika saa nane mchana. Tunatarajia kuwa na wageni waalikwa takribani 500. Siku ya kwanza mdahalo utafunguliwa na Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud,” ameeleza Dkt. Senkoro na kuongeza, 

“Siku ya pili tarehe 14 Julai itakuwa Siku ya kilele cha mdahalo huu kwa mwaka 2022 na Mgeni Rasmi katika Siku hii muhimu atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh. Samia Suluhu Hassan,”.

Kwamba Viongozi wengine wa kitaifa watakaohudhuria mdahalo huu ni pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye pia ni msarifu wa Taasisi hiyo, aliyerithi nafasi ya Hatari Benjamin Mkapa kuanzia Desemba mwaka jana.
 
Wageni wengine watakaoshiriki hafla hiyo ni pamoja na Viongozi wakuu wa Serikali, Marais na Viongozi wastaafu kutoka Tanzania Bara na Visiwani, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, wakuu wa mashirika ya kimataifa nchini, wakuu wa Taasisi mbalimbali za Sekta binafsi na Umma, wanafamilia na marafiki wa Hayati Benjamin Mkapa kutoka ndani na nje ya nchi, pamoja na Asasi za Kiraia na Viongozi wa Dini.