ACT WAZALENDO YATOA MAPENDEKEZO 4 KWA WIZARA YA KILIMO.
Hali ya upatikanaji na mgawo wa pembejeo za korosho; Uzalishaji wa korosho unawekwa matatani.
Utangulizi
Mwezi Mei mwaka huu, katika kipindi cha uwasilishaji wa bajeti za wizara katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali ilitangaza uamuzi wa kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima wa mazao yote nchini ikiwemo na zao la korosho.
Uamuzi huo ulitangazwa na waziri wa Kilimo, ndugu Hussein Bashe mbele ya Bunge. Waziri Bashe aliongezea kuwa uamuzi huo ni kutokana na serikali kuamua kutumia ushuru wa kusafirisha korosho ghafi (Export levy) kuendeleza zao la korosho ni dhambi kuwachangisha tena na alithibitisha kuwa Serikali itawapatia wakulima wote pembejeo za kutosha.
Kutangazwa kwa uamuzi huu kuliibua matarajio na matumaini makubwa sana kwa wakulima wa korosho ambao walifurahia kupunguziwa mzigo wa kununua pembejeo ambazo tayari zimeonyesha kupanda kutokana na mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali nchini.
Aidha, uamuzi huu wa serikali uliondosha utaratibu wa awali ulipangwa na serikali wa wakulima kuchangia nusu bei ya pembejeo kupitia vyama vya ushirika na nusu inayobaki kugharamiwa na serikali.
Pili, wakulima kutumia fedha zao walizotunza kwa ajili ya kununua dawa za salfa na viuatilifu vingine kutokana na tangazo la serikali kutoa pembejeo bure. Tatu, wafanyabiashara binafsi walisita
kuagiza pembejeo za korosho kwa kuhofia kukosa soko.
ACT Wazalendo tumefuatilia kwa karibu sana mwenendo wa usambazaji na mgawo wa pembejeo hizi kwa wakulima wa korosho kwenye mikoa ya Ruvuma (Tunduru), Lindi na Mtwara, Kinyume na ahadi ya serikali ya kuleta pembejeo ya bure, ya kutosha na kwa wakati, hali imekuwa tofauti mno. Kuna
matatizo makubwa yametokea kama ifuatavyo;
1. Kucheleweshwa kwa pembejeo.
Kwa kawaida wakulima wa korosho wanaanza kupuliza mwezi wa tano (Mei) Lakini cha kushangaza hadi leo tarehe 30 June 2022 kasi ya usambazaji ni ndogo mno mfano katika wilaya ya Tunduru yapo maeneo kama vile tarafa ya Namasakata, Lukumbule na Nalasi hawajapokea. Hali hiyo ipo pia kwenye wilaya za Liwale, Kilwa, Newala na Mkoa Mzima wa Pwani.
2. Pembejeo zilizotolewa ni kiduchu mno.
Pamoja na kucheleweshwa kwa usambazaji wa pembejeo kwa wakulima kwenye baadhi ya maeneo, lakini inaumiza na kushangaza kuona kiwango kilichotolewa na kupangwa kutolewa ni kiduchu mno.
Mahitaji ya kitaalamu kwa kila mkorosho unahitaji kilo 1 na robo kwa mizunguko mitano. Lakini, kiasi kilichotoelwa mathalani mkulima anayetumia mifuko 50 kwa mwaka anapewa mifuko 2. Kwa mfano chama cha Msingi LIMA hakuna mkulima aliyepewa mifuko ya sulphur zaidi mitatu (3). Inashangaza sana kuona serikali inajua mahitaji halisi kwa kila mkulima kutokana na taarifa zilizopo, lakini inatoa pembejeo ambazo hamziwasaidii wakulima badala yake kuua kilimo chenyewe.
3. Utaratibu mbovu za usambazaji.
Waziri alitoa maagizo yote kwa viongozi wa vyama vya Ushirika, wakulima wakivuna korosho hulazimika kuziuza kupitia vyama vya Ushirika. Ni vyama hivyo ndivyo vinavyowafahamu wakulima wote wa maeneo wanayofanyia kazi. Cha kustaajabisha, mgao wa pembejeo kwa Tunduru unasimamiwa moja kwa moja na Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya ni Mwenyekiti wa Kamati ya pembejeo Wilaya. Kama inavyofahamika, Mwenyekiti wa Kamati siyo mtendaji, kama kulikuwa na ulazima wa kusimamia viongozi wa serikali, basi watendaji katika ngazi ya serika wilaya ni Mkurugenzi na Wakuu wake wa Idara. Athari za uingiliwaji huo wa dola, umeleta usumbufu mkubwa sana kwenye zoezi zima la usambazaji wa pembejeo hizo.Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haina wataalamu wa Usafirishaji na Usambazaji (Transport and Logistics) hata uzoefu wa kufanya kazi hizo pia hawana.
4. Uhaba wa pembejeo umepaisha bei zaidi.
Baada ya tamko la serikali la kuwapatia wakulima pembejeo za bure, wafanyabiashara wengi waliamua kutojishughulisha na uagizaji wa pembejeo za korosho. Wachache waliofanikisha kuleta, wanaziuza kwa bei kubwa. Kwa mfano, sulphur ya chapa ya mtende toka Saudi Arabia inauzwa Shilingi 55,000 hadi 60,000 badala ya bei ya tshs 36,000.
5. Hofu ya pembejeo bandia (zisizo na ubora).
Katika Mkoa wa Mtwara zilisambazwa pembejeo feki, wakulima washtukia mapema kabisa, serikali ilichukua hatua kwa kuzikamata. Lakini hadi sasa, hakuna taarifa za uwazi za hatua zilizochukuliwa kwa Wafanyabiashara hao na salfa iliyokamatwa haijulikani imepelekwa wapi. Wananchi wanahofia inaweza ikawekwa kwenye mzunguko wa biashara tena.
i wa korosho nchini, itapunguza kipato cha
wakulima na kuwaingiza kwenye ufukara. Kutokana na hali hiyo, ACT Wazalendo kinatoa wito kwa serikali kuchukua hatua zifuatazo:
1. Serikali itumie taarifa zilizopo za wakulima (ukubwa wa mashamba) katika kutimiza ahadi yake ya kugawa pembejeo bure kwa wakulima kulingana na mahitaji halisi. Serikali iimarishe mfumo wa usambazaji kupitia vyama vya ushirika vya korosho (AMCOS).
2. Serikali itoe taarifa za uhakika mapema kuhusu upatikanaji wa pembejeo badala ya kutoa taarifa za hadaa. Kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakijinunulia pembejeo wenyewe. Ni bora serikali ieleze wazi juu ya uwezo wake ili wakulima waweze kujiandaa mapema kwa kujiwekea akiba kwa ajili ya kununua pembejeo.
3. Serikali iweke wazi hatua zilizochukuliwa dhidi ya Wafanyabiashara walikamatwa na pembejeo bandia, ili kuondosha wasiwasi wa wananchi.
4. Ili kuziba pengo la mahitaji ya pembejeo kwa wakulima wa korosho serikali inunue salfa na viuatilifu vyote kutoka kwa Wafanyabiashara wote kisha isambaze kwa wakulima. Hii itawalinda wakulima kutokana na kulanguliwa kwa bei ya juu na kudhibiti ubora wa pembejeo.
Mwisho; ni dhahiri kuwa Serikali inarudia tena makosa iliyofanya mwaka 2017, ya kuwaadaa wakuliwa wa korosho kwa ahadi hewa, zinazoenda kuharibu mfumo imara wa wakulima wenyewe kupata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu. Sisi, ACT Wazalendo tunaendelea kusisitiza kuwa Serikali ni lazima itimize wajibu wake wa kulinda maisha na hali za wananchi kwa kuhakikisha hakuna uhaba wa pembejeo kwa wakulima hawa wa korosho nchini, kuhakikisha kuwa pembejeo husika zinapatikana katika bei ambayo watanzania wanaimudu, na zinapatikana kwa wakati.
Imetolewa na;
Ndugu Mtutura Abdallah Mtutura,
Waziri Kivuli wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi




