Breaking News

TAA WAINGIA MAKUBALIANO NA MACHINGA KUWAJENGEA UWEZO

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Makundi Maalum Mhe. Amon Mpanju akionyesha hati za makubaliano kati ya Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) na shirikisho la umoja wa wamachinga taifa (SHIUMA) iliyofanyika jijini Dar es salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Makundi Maalum Mhe. Amon Mpanju akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano kati ya Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) na shirikisho la umoja wa wamachinga taifa (SHIUMA) iliyofanyika jijini Dar es salaam
Mwanasheria wa Serikali, Bi Tabitha Dida akilezea namna makubaliano hayo kati ya Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) na shirikisho la umoja wa wamachinga taifa (SHIUMA) iliyofanyika jijini Dar es salaam.

Dar es Salaam:
Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum wameingia makubaliano ya kuwawezesha na kuwajengea uwezo wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama Machinga.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa Makubaliano hayo jijino Dar es salaam Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Makundi Maalum Mhe. Amon Mpanju amesema makubaliano hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo wa kujisimamia kifedha na kukua.

Mhe. Mpanju amesema hiyo ni fursa kwa wamachinga waitumie vizuri wakati wakisubiria Serikali ikiwa katika mchakato wa kuanda sheria na sera ya Wafanyabiashara ndogo ndogo.

“Tunahitaji TAA waingie watusaidie ili tupate kanzidata zilizo sahihi ambazo zitasaidia kuwatambua na kuwawekea mazingira rafiki kuwawezesha kufanya biashara zenu kwa ufanisi hivyo kuongeza pato lenu na taifa" Alisema Mhe. Mpanju.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa shirikisho la umoja wa wamachinga taifa (SHIUMA) bwana Ernest Matondo amesema kupitia ushirikiano huu utawasaidia kufanikisha shughuli zao za kimachinga hivyo kuiomba Wizara ibadilishe baadhi ya Sheria kuwawezesha kupata mamlaka na ambazo halmashauri wanazo hivyo kupelekea kutambulika rasmi.

Nae Makamu mwenyekiti Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), bwana Victorious Kamuntu amesema lengo kubwa la makubaliano haya ni kuwawezesha wafanyabiashara hao na makundi maalumu kuwezeshwa na wadau mbalimbali kukuza biashara zao.

“Mradi unalenga watu wa chini kabisa namna gani watakuza biashara na uchumi wa nchi, sisi tunaangalia sera na kushauri Serikali ili SHIUMA wakue wafike juu ” Alisema Bw. Kamuntu.

Awali Mwanasheria wa Serikali, Bi Tabitha Dida amesema TAA ina madhumuni ya kujengea uwezo wafanyabiashara ndogo ndogo pande zote mbili zimeingia makubaliano ili kukuza biashara za Machinga.

"Chama cha Wahasibu kupitia mpango huu kina dhamira ya dhati kuwasaidia wafanyabiashara ndogo ndogo nchini kuwawezesha kutambulika na kupatiwa misaada kutoka kwa wadau pamoja na serikali" Bi. Dida.