BILIONI 6 ZATUMIKA UJENZI WA JENGO LA OFISI YA MKUU WA MKOA WA MBEYA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akifungua jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa wa mbeya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ameridhishwa matumizi ya fedha za ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya lililogharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.
Ametoa kauli hiyo leo Agosti 5, 2022 wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo hilo kwenye ziara yake ya siku Nne ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini Mbeya.
Amesema kuwa katika suala la utawala bora Serikali ya awamu ya sita inaboresha maeneo ya wananchi ili waweze kupata huduma kwenye mazingira bora halkadhalika na wale wanaotoa huduma waweze kufanya kazi katika mazingira bora na kuhusumia jamii kwa moyo.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha na kujenga majengo ya Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Majengo ya Halmashauri,nyumba za wakuu wa Wilaya lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya kutoa huduma bora kwa jamii.
“Utafiti unaonyesha kuwa tunapofanya kazi kwenye mazingira mazuri, utoaji wa huduma hutolewa vizuri hivyo Serikali imeamua kutumia fedha nyingi kujenga Ofisi za Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Samia amesema Serikali itaendelea kujenga majengo kama hayo katika Mikoa yote hasa katika maeneo ya Kikanda.
Aidha, Mheshimiwa Samia amesema kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo amewataka Madiwani kuhakikisha wanasimamia fedha hizo ili ziweze kutekeleza miradi iliyokusudiwa na Serikali.







