Breaking News

NAIBU WAZIRI KATAMBI AWATAKA WANUFAIKA WA MIKOPO YA SERIKALI KUIREJESHA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) mheshimiwa Patrobas Katambi, akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea kilele Cha siku ya Kimataifa ya Vijana inayoadhimishwa Kila mwaka Agosti 12 duniani.

Muwakilishi mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi, Bwana Wilfred Ochana akiongea na waandishi wa habari kuelekea kilele Cha siku ya Kimataifa ya Vijana inayoadhimishwa Kila mwaka Agosti 12 duniani.

Dar es salaam:
Serikali imewataka vijana kote nchini ambao ni wanufaika wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili vijana wengine waweze kunufaika.

Aidha ameziagiza halmashauri zote nchini kutenga asilimia nne ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwapatia vijana mitaji ya kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali.

Akizungumza jijini Dar es salaam Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) mheshimiwa Patrobas Katambi, kuelekea kilele Cha siku ya Kimataifa ya Vijana inayoadhimishwa Kila mwaka Agosti 12 ambapo mkutano huo umeandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA)

Mhe. Katambi amesema serikali imekuwa ikitenga kiasi Cha shilingi billion moja kila mwaka kwa ajili ya mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana.

Amesema mikopo hiyo hutolewa na Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kwamba mpaka sasa Sh bilion 3.2 zimetolewa kwa vikundi vya vijana 586 vyenye wanachama 4,222 kwenye halmashauri za Wilaya 155.

“Kumekuwa na changamoto kubwa ya vijana wengi kutorejesha mikopo kwa wakati jambo ambalo linasababisha vijana wengine kushindwa kunufaika na mikopo hiyo. Nawasihi vijana wenzangu kurudisha mikopo ili na wenzetu waweze kunufaika,” alisema Katambi.

Pia amesema halmashauri za wilaya zinapaswa kutenga maeneo maalum ya shughuli za kiuchumi kwa vijana na kuwekewa miundo mbinu na huduma muhimu kwa jamii kama vile; barabara, maji, umeme, vyoo, huduma za Afya, huduma za fedha na huduma za hifadhi ya jamii.

Kwa mujibu wa Katambi, Mkoa wa Dar es Salaam pekee ulitoa zaidi ya Sh bilioni 50 kwa ajili ya mikopo kwa vikundi na kwamba fedha zilizorudishwa ni Sh bilioni 10 pekee.

“Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaoesha kuwa kati ya watu bilioni nane duniani kote, idadi ya vijana ni bilioni 1.8 na matokeo ya utafiti wa nguvu kazi ya taifa ya mwaka 2020/21 yanaonesha kuwa, idadi ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 inakadiriwa kufikia watu milioni 18.3 kati yao, vijana wenye uwezo wa kufanya kazi ni milioni 14.6 sawa na asilimia 80,” amesisitiza

Kwa upande wake Naibu Muwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi Wilfred Ochana,amesema UNFPA Tanzania itaendelea kuwasapoti vijana nchini ili waweze kufikia malengo yao ikiwemo kuanzisha pogramu za vijana.

“Tunafahamu kuwa vijana wa kitanzania ni wabunifu,wajasiriamali na viongozi katika jamii zao ,tunatazamia kuendelea kuona na kuunga mkono vijana ili kutimiza na kupanuka katika jukumu hilo,”amesema Wilfred Ochan.

Aidha, Bwana Ochan amewahimiza vijana kujitokeza katika kushiriki katika sensa ya watu na makazi Agoust 23 mwaka huu kwakuwa sensa ni muhimu ili kufanikisha ugawaji wa rasilimali na Uundaji wa Sera, ikiwa ni pamoja na sera zinazowalenga vijana na upangaji programu ambazo wao wanazileta.