MAMLAKA YA SERIKALI MTANDAO YAWAJENGEA UWEZO VIJANA WA VYUO VIKUU ILI KULETA MAENDELEO YA TEHAMA NCHINI
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akfafanua jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kuwajengea uwezo wanafunzi wq vyuo vikuu utakaosaidia kuleta maendeleo ya TEHAMA nchini yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)
Washiriki wa mafunzo hayo kutoka vyuo vikuu mbalimbali wakifatilia hotuba ya mgeni rasmi.
******"
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imewapatia mafunzo ya TEHAMA vijana wa vyuo vikuu ili kuwajengea uwezo utakaosaidia kuleta maendeleo ya TEHAMA nchini ikiwa ni pamoja na kuwaandaa vijana hao kutoa mchango katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Mhe. Ndejembi amesema hayo jijini Dodoma, wakati akifunga mafunzo ya TEHAMA kwa vijana hao wa vyuo vikuu yanayotolewa kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA). Naibu Waziri Ndejembi amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeelekeza nguvu nyingi katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambao unahitaji wataalam na ndio sababu ya serikali kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa vijana ya vyuo vikuu.
“Ninyi vijana mliopatiwa mafunzo kupitia kituo hiki cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha eGA ndio wataalam mnaotegemewa kutoa mchango ili kufikia lengo la Mhe. Rais la kuwa na Tanzania ya Kidijitali,” Mhe. Ndejembi amesisitiza. Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, uwepo wa kituo hicho cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na kituo kitakachokuwa ni kitovu cha kukuza vipaji katika eneo la TEHAMA.
Mhe. Ndejembi ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kuanzisha kituo hicho kitakachosaidia kufikia lengo la Mhe. Rais la kuzalisha wataalam wengi wa TEHAMA ambao watakaotoa mchango katika kubuni mifumo imara itakayoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba amesema, suala la utafiti na ubunifu limepewa kipaumbele na eGA katika kuendeleza jitihada za serikali mtandao ndio maana ilianzisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo ya TEHAMA ambacho ndani ya muda mfupi kimekuwa na faida katika kukuza vipaji vya vijana wa Vyuo Vikuu kwenye eneo la TEHAMA.





