Breaking News

BRELA YAWAHAMASISHA WAFANYABIASHARA ARUSHA KURASIMISHA BIASHARA ZAO

NA MWANDISHI WETU
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni  (BRELA), imetoa wito kwa wafanyabiashara ambao  bado hawajarasimisha  biashara zao kufanya hivyo ili  kuepuka changamoto mbalimbali za kibiashara.

Wito huo umetolewa leo tarehe 13 Desemba, 2023 na Ofisa Sheria kutoka  BRELA, Edward Magayane, kwenye banda la BRELA  nje ya Ukumbi  wa Mikutano wa Kimataifa (AICC), jijini Arusha, linakofanyika  Kongamano la 14 la mwaka la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi.

Aidha, Magayane amesema katika kipindi cha kongamano, Maafisa wa BRELA  wanatoa mwongozo kwa wadau wanaotembelea banda hilo juu ya mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS).

 Pia ameongeza kuwa mfanyabiashara anaporasimisha biashara yake, humuwezesha kupata fursa  mbalimbali ikiwemo mikopo kutoka  taasisi za kifedha, kupata zabuni zinazotangazwa serikalini na nyinginezo.

"Tunatoa ushauri  na elimu kwa wadau wanaotembelea banda letu na wanaotaka kusajili kampuni na huduma nyingine wafike  kwenye banda letu tutawapatia usaidizi," amesema Magayane.                   

Kongamano hilo lililoanza tarehe 12 Desemba litahitimishwa kesho, Desemba14 , 2023