RAIS SAMIA KUFUNGUA MKUTANO WA DIRA MPYA YA MAENDELEO YA TAIFA DEC, 9 JIJINI DAR
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Dira mpya ya Maendeleo ya taifa ya mwaka 2050 utakaofanyika Disemba 9 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
Akizungumza Jijini Dar es saalam Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema Mkutano huo utazindua, kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za kitafiti na Tathimini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ikiwa ni pamoja na mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa dira hiyo iliyoanza kutekelezwa tangu mwaka 2000.
Ameongeza kuwa Mkutano huo utahudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka nchi nzima takribani watu 971 wakiwemo Viongozi Serikali ,Vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Taasisi mbalimbali, Wazee, Vijana, Makundi maalumu na Makundi mengi kwenye jamii.
Aidha amesema katika Dira ya maendeleo ya 2025 Tanzania imefanikiwa kufikia asilimia 124% ya kujitosheleza kwa chakula ikilinganishwa na lengo la kufikia asilimia 140% ifikapo mwaka 2025,Mtandao wa barabara za lami na zege (paved road) katika mikoa umeongezeka kutoka Km 4,179 mwaka 2000 hadi Km 11,966.38 mwaka 2023 huku idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi vikipungua kutoka vifo 760 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2000 hadi kufikia vifo 104 mwaka 2022 ikiwa tumevuka lengo la kufikia vifo 265 ifikapo 2025.
Ameongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo taarifa ya tathimini inaonyesha kuwa pato la Mtanzania (GDP per capital income limeongezeka kutoka dola za kimarekani 399.5 (TZ 322,597) mwaka 2000 hadi kufikia dola za Kimarekani 1200 (TZ 2,880,000) mwaka 2022.
"Katika huo mkutano Mheshimiwa Rais atazindua rasmi Timu kitaifa ya Kitaalamu ya kuandaa na kuchakata Dira ya maendeleo 2050 (National Vision Core Technical Team) na kamati ya Usimamizi wa Dira hiyo (National Vision Steering Commitee) pamoja na nyenzo za kidigitali zitakazotumika katika kukusanya maoni ya wadau,kumeandaliwa vifaa vya kisasa vitavyomwezesha mwananchi kutoa maoni popote alipo kwa kutumia njia za kidigital" Alisema Profesa Mkumbo.
Mkumbo amewataka Wananchi na kuwasisitiza kufuatilia mchakato wa kuandaa Dira mpya ya maendeleo ya 2050 na kushirikia kikamilifu katika kutoa maoni yao kuhusu Tanzania waitakayo katika miaka ijayo na kusisitiza kuwa maoni yote yatazingatiwa.
"Kwa kuzingatia maelekezo ya Mh Rais Kwamba zoezi la kuandaa dira mpya ya maendeleo liwe jumuishi na shirikishi,mkutano huu utahusisha makundi yote na watu wote nchi nzima".




